Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imetupa pingamizi la mawakili wa Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema la kuitaka isisikilize kesi ya
kuhamasisha maandamano ya Ukuta, bali kwanza ifikishwe Mahakama ya
Katiba.
Lema, ambaye ni mbunge kupitia Chadema, anakabiliwa na kesi hiyo
akidaiwa kuhamasisha maandamano hayo ya chama chake yaliyokuwa
yamepangwa kufanyika Septemba Mosi, mwaka jana.
Mawakili wa Lema, John Mallya na Sheck Mfinanga, waliwasilisha ombi
mahakamani hapo wiki iliyopita wakitaka kesi hiyo isikilizwe Mahakama ya
Katiba kwa kuwa kuna hoja za kikatiba ambazo zitahitaji kutolewa
maelezo na majaji watatu wa Mahakama hiyo.
Katika kesi hiyo, Lema anadaiwa kuhamasisha maandamano kwa njia ya
mtandao wa kijamii (audio clip) aliyoitengeneza na kujirekodi ujumbe
mfupi wa sauti na kisha kusambaza Agosti Mosi hadi 26, mwaka jana
katika mitandao ya kijamii ya WhatsApp.
Hakimu Bernard Nganga alisema kosa alilofanya Lema siyo la kikatiba na
hoja za kutaka kuhamishiwa shauri hilo Mahakama ya Katiba hazina mashiko
kisheria.
Alisema sheria ipo wazi, kuwa mtu yeyote akihusika na kushawishi
utendaji wa kosa hata kama halina madhara, muhusika ana makosa na adhabu
yake ni kifungo cha miaka miwili au kulipa faini.
Hakimu Nganga alisema pingamizi za utetezi zimetupwa na shauri litaendelea kusikilizwa.
Tags
SIASA
