Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa
Kusini mwa Tanzania (Saggot), Geoffrey Kirenga amesema kama kuna jambo
linaloumiza ni Australia kutumia nyasi kutoka Tanzania kwa ajili ya
malisho na kisha kurejesha maziwa na nyama kutuuzia hapa nchini.
Kirenga amesema hayo wakati akizungumzia namna Tanzania ilivyo fursa
nyingi ambazo zimeachwa bila kuendelezwa au kushughulikiwa na wananchi
ili kuwezesha Taifa kuendelea.
“Lakini cha kushangaza, Australia wanatumia nyasi za Tanzania kulisha
ng’ombe wao halafu wanakuja kutuuzia nyama na maziwa,” amesema.
Ameongeza kuwa,“vilevile tuna tatizo la kuhifadhi chakula, mahindi
yanayozalishwa nchini kwa mwaka ni kati ya tani milioni 6 hadi 7, lakini
yanayohifadhiwa kwa njia za kisasa ni kati ya tani milioni moja hadi
mbili yaliyobaki yanahifadhiwa kwa njia za kienyeji, yanaishia
kuharibika. Ipo haja kwa Serikali ikatengeneza maghala katika maeneo ya
uzalishaji.”
Kirenga akasema katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania ina
fursa nyingi za kilimo lakini tatizo ni kukosa uthubutu na taarifa za
uhakika.
Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Saggot, Jennifer Baarn amesema wanaangalia
matatizo yanayorudisha nyuma sekta ya kilimo na namna ya kuyatatua ili
kuhakikisha mnyororo wa kuongeza thamani ya mazao unaleta tija kwa
wakulima, hasa wadogo.
Tags
HABARI KITAIFA
