Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Mara, Livingstone
Gamba amesema licha ya walimu kupiga kelele kila mara, Serikali imekaa
kimya kuhusiana na malimbikizo ya madai wanayoidai.
Gamba amesema wataendelea kupiga kelele bila kuchoka kwa kuwa wanachodai
ni haki yao ya msingi na kwamba, jasho lililowatoka ndilo
wanalolipigania.
Wakati kigogo huyo akisema hayo, Chama cha Walimu Tanzania (CWT)
wilayani Tarime kimetangaza ‘mshiko’ wanaoidai Serikali umefikia Sh399
milioni.
Akizungumza kwenye mkutano wa kamati tendaji ya chama hicho wilayani
Tarime, Mwenyekiti wa CWT wa wilaya hiyo, Shirikisho Nyagoseima amesema
madai hayo ni matibabu (Sh30 milioni), likizo (Sh20. 6 milioni), masomo
(Sh22.7 milioni), uhamisho (Sh183.8 milioni), mazishi (Sh6.3 milioni),
usafirishaji mizigo (Sh20 milioni) na mishahara yanayofikia Sh245.3
milioni.
“Tunaitaka Serikali kulipa stahiki hizi ili walimu wafanye kazi kwa
kiwango kinachotakiwa ifikapo Machi Mosi ili tusiingie kwenye mgogoro,”
amesema Nyagoseima.
Tayari Rais wa CWT ngazi ya Taifa, Gratian Mkoba ametangaza kuwa chama
hicho kinatarajia kutangaza mgogoro na Serikali ifikapo mwezi ujao iwapo
malimbikizo ya madai ya walimu yatakuwa hayajalipwa.
Tags
ELIMU
