Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akisisitiza jambo kwa waandishi wa
habari, (hawapo pichani), mara baada ya kukagua ujenzi wa Jengo la tatu
la Abiria (TB III), jijini Dar es Salaam.
Mafundi wa Kampuni ya BAM
wanaojenga jengo la tatu la Abiria (TB III) wakiendelea na kazi ya
ujenzi, jijini Dar es Salaam. Kazi ya ujenzi zimeanza baada ya
kutarajiwa kusimama sababu ya kukosekana fedha ambapo Serikali imesema
itatoa fedha za kukamilisha mradi huo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kushoto), akitoa maelekezo kwa timu
aliyoiteua kusimamia ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria (TB III), mara
baada ya kuteuliwa leo jijini Dar es Salaam.
………
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameteua timu mpya ya wataalamu saba
kwa ajili ya kusimamia mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria
(Terminal III), katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius
Nyerere.
Hatua hiyo imefikiwa kufuatia
agizo la Mheshimiwa Rais John Magufuli alilolitoa jana wakati alipofanya
ziara ya kushtukiza uwanjani hapo kujionea maendeleo yaliyofikiwa
katika mradi huo.
Timu hiyo inaongozwa na Eng.
Julius Ndyamukama inaundwa na Eng, Godson Ngomuo, Eng. Humphrey
Kanyenye, Eng. Abednego Lyanga, Eng. Mbila Mdemu na Eng. Rehema Myeya.
“Naamini timu hii ina wataalamu
mahiri, hivyo itasimamia ujenzi huu kukamilika kwa wakati na kwa
kuzingatia thamani ya fedha (value for money”, amesema Waziri Mbarawa.
Profesa Mbarawa amemhakikishia
mkandarasi wa kampuni ya BAM kutoka uholanzi inayojenga jengo hilo kuwa
Serikali itamlipa mkandarasi huyo katika kipindi cha wiki mbili kutoka
sasa.
Aidha, ameitaka timu hiyo kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo unakamilika mwezi Desemba mwaka huu kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake Meneja wa mradi
huo Eng. Julius Ndyamukama, ameahidi kushirikiana na wenzake katika
kuhakikisha mradi huo unamalizika kwa wakati.
Kiasi cha Shilingi Bilioni 560 zinatarajiwa kutumika katika kugharamia ujenzi huo kwa awamu zote mbili.
Katika hatua nyingine Profesa
Mbarawa amemsimamisha kazi Meneja wa Fedha kutoka Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege nchini (TAA) Bw. Simba Lugando kwa kuidhinisha malipo ya ujenzi
wa Uwanja wa ndege wa Songwe mkoani Mbeya kwa mkandarasi wa Kampuni ya
DB Shapriea kiasi cha shilingi Bilioni 3.3 ambapo ujenzi wake
haukufanyika ipasavyo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Tags
MIUNDOMBINU