BANDA MEDIA BLOG

Sekta ya Ujasiriamali ndiyo silaha pekee ya kupambana na umaskini wa kipato nchini


jk1NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR.
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema sekta ya Ujasiriamali  ndiyo silaha ya pekee ya kupambana na  changamoto za umaskini wa kipato nchini.
Alisema bila ya kujali tofauti za kijinsia kila mwananchi visiwani Zanzibar anatakiwa kuchangamkia fursa zinazotokana na sekta hiyo kwa kujifunza utaalamu wa kutengeneza bidhaa mbali mbali teknolojia rahisi na isiyokuwa na gharama kubwa.

Hayo aliyasema Kaimu Katibu Mkuu wa umoja huo Taifa, Shaka Hamdu Shaka wakati akizindua Mafunzo ya ujasiriamali ya utengenezaji wa Bidhaa za vitenge, vikoi, mishumaa ya dawa za mbu, chaki na usindikaji wa matunda na mboga mboga kwa vikundi vya Akina Mama wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Shaka aliwasihi akina mama hao kufuatilia kwa makini mafunzo hayo ili wapate ujuzi wa kudumu utakaosaidia kuwafundisha wanawake wengine katika maeneo mbali mbali nchini.
 Aliwataka Wanawake  katika Mkoa huo kuchangamkia fursa hizo ili kutekeleza kwa vitendo dhana ya maendeleo kupitia sekta ya viwanda vidogo vidogo ndani ya Mkoa huo.
Alisema hatua za kufikia malengo hayo ni lazima wajenge  utamaduni wa kujikusanya pamoja katika vikundi sambamba na kujiamini na kuaminiana miongoni mwao kwa kuanzisha miradi kupitia rasilimali chache walizokuwa nazo kwani itakuwa rahisi kupatiwa nyenzo za kiutendaji kutoka serikalini na kwa viongozi wa majimbo.
 Alisema Zanzibar bado haijatumia vizuri fursa za ujasiriamali na vikundi vya ushirika hali inayosababisha kuwepo na malalamiko mengi ya ukosefu wa ajira wakati kuna njia mbadala ya wananchi kujiajiri wenyewe kupitia sekta hizo kwa lengo la kujipatia kipato na kupunguza ukali wa maisha.
“ Huu ndio wakati mwafaka wa kutengeneza Mkoa wa Kaskazini Unguja wenye Viwanda kupitia sekta za ujasiriamali, hivyo tumieni vyema fursa hii kwani nyinyi ndio shamba darasa mtakaoweza kutoa elimu katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba ili kila mwanamke na makundi mengine waweze kunufaika na ujuzi huo”., alisisitiza Shaka.
Ametoa wito kwa akina mama hao kutengeneza bidhaa bora na zenye viwango zitakazoweza kuingia katika soko la ushindani wa kibiashara ndani na nje ya nchi.
Aidha alieleza kuwa fursa hizo zinatokana na utekelezaji wa ahadi zilizotolewa katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita sambamba na usimamizi mzuri wa sera na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Kaimu Katibu Mkuu huyo, alimpongeza Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa huo, Mh. Angelina Adam Malembeka kwa ubunifu wake wa kuwasogezea karibu wananchi wake fursa za kimaendeleo na kuwataka viongozi wengine wa kisiasa nchini kuiga mambo mema kutoka kwa kiongozi huyo.
Aliwataka Akina Mama hao kuwa karibu na vijana ili kundi hilo liweze kunufaika na fursa hizo, ambapo Shaka aliahidi awamu ijayo ya mafunzo hayo kuwadhamini vijana 100 wa UVCCM nao kupatiwa taaluma hiyo.
Akizungumzia suala la Uchaguzi wa CCM na Jumuiya zake unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, alisema ili kujenda chama kipya na Tanzania mpya kwa vitendo ni lazima kufanyike mabadiliko makubwa ya kupatikana viongozi na watendaji wenye vigezo vya uzalendo, weledi na wasiokuwa na chembe chembe za usaliti na ufisadi wa kurejesha nyuma maendeleo ya taasisi hizo.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa huo, Angelina  Adam Malembeka alisema mpango wa kutoa mafunzo hayo kwa akina mama wa Mkoa huo yatafanyika kwa awamu nne tofauti kwa kipindi cha mwaka mzima na yatakuwa endelevu chini ya ufadhili wake.
Alisema zaidi ya vikundi nane vilivyoanda mafunzo hayo ambao ni Makatibu na Wenyeviti wa ngazi za Mashina wa UWT  kila kikundi kilipatiwa kiasi cha shilingi 100,000 kwa ajili ya kufungua acounti za benki na sh.300,000 kwa ajili ya fedha za kununulia vifaa vya kuanzia mafunzo.
Hata hivyo shaka kupitia kikao hicho aliahidi kutoa sh. Milioni moja kama sehemu ya kuwapa hamasa akina mama kwa lengo la kuzidisha juhudi katika mafunzo yao.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG