ASKARI wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Sajini John
Komba na wenzake wanne wakiwemo mgambo na wanafunzi wa jijini hapa,
wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga kwa kosa la
kusababisha kifo cha aliyekuwa kondakta wa daladala inayosafiri kati ya
Nguvumali na Raskazoni, Salim Kassim (18) mkazi wa Mwamboni.
Wakili wa Serikali, Donata Kazungu akisoma shitaka hilo la mauaji
linalowakabili watuhumiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Hilda
Lyatuu alisema Januari 26, mwaka huu katika Kambi ya JWTZ iliyoko Kata
ya Nguvumali jijini Tanga, Komba mwenye namba MT 69500 na wenzake watatu
walimuua Kassim katika eneo la kambi hiyo.
Wakili Kazungu aliwataja washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Adam
Juma (20), Sofia John (20) ambao ni mwanafunzi, Yohana Warioba na
Bernard Nicholaus ambao ni wanamgambo wanaolinda katika kambi hiyo.
Hata hivyo, watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na
mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji. Aidha,
upelelezi kuhusu kesi hiyo haujakamilika na hivyo itatajwa tena Februari
26, mwaka huu.
Tags
UKATILI
