WATU wengi walipigwa na butwaa na kubaki midomo wazi baada ya kuvuja kwa
sauti inayodaiwa kuwa ni ya mchekeshaji Steve Mengere ‘Steve Nyerere’
na mama mzazi wa muigizaji Wema Sepetu.
Audio ilikuwa ya kawaida tu, lakini kilichofanya ionekane ishu, ni kule
kuwahusisha watu wazito kwenye nchi hii na sakata la kukamatwa na
baadaye kushtakiwa kwa matumizi ya bangi, kwa Wema. Kama ilivyotarajiwa,
Steve Nyerere alitumia uungwana, akatoka mbele ya jamii na kuomba
radhi.
Hicho ndicho kitu pekee ambacho alipaswa kukifanya, vinginevyo angekuwa
mtu wa ajabu ‘kukausha’ ili kuacha upepo upite kama pepo zingine
zinavyopita. Na niseme ukweli, utetezi wake pia nimeupenda, maana
amesema kweli kuwa ilibidi atumie sanaa ili kumuweka vizuri mama ambaye
aliishi naye vizuri kama mwanaye.
Ni vile tu mama Wema aliwahi kusema, lakini hata mimi nilikuwa najiuliza
kwa kutomuona Steve akienda kumsabahi dada yake pale Central au hata
kumsindikiza mahakamani. Historia inanionyesha huyu mchekeshaji huwa
hakosi katika matukio yanayomhusisha Wema Sepetu na mara kadhaa,
ameonekana akiwa karibu na mama Wema. Yes, ilibidi atumie sanaa ili
kumuweka sawa na alifanikiwa.
Kwa hiyo, alichojaribu kusema ni kuwa yote aliyoongea ndani ya sauti
ile, ni uongo. Kwamba hakwenda Dodoma, hakuongea na mawaziri waliotajwa
wala wabunge na kwamba kilichotokea hakihusiani kwa namna yoyote na
yeye. Lakini katika uhalisia wake, kuna uhusiano mkubwa wa kilichosikika
na kilichotokea, ingawa siyo hoja ya leo hapa.
Ninachotaka tuwekane sawa, ni namna gani Steve Nyerere anapata mkate
wake wa kila siku. Ukimsikiliza wakati akizungumza na waandishi wa
habari, alisema yeye anaishi kwa sababu ya jina lake, alilotumia miaka
mingi kulitengeneza. Steve ni muigizaji wa filamu na mchekeshaji. Huku
kwenye filamu hajawahi kuwa staa wa kuuza sana kiasi cha kusema anaishi
maisha tunayomuona kwa sababu hiyo.
Lakini pia kwenye uchekeshaji, siku hizi kuna kitu kinaitwa Stand Up
Comedy, ile ambayo msanii anawajaza watu ukumbini na yeye kuanza
kuwachekesha. Wanafanya hivi pia waigizaji wengine ambao kwa Afrika
Mashariki, kinara wao ni Eric Omondi wa Kenya, Anna Kasiime wa Uganda na
hapa nyumbani, MC Pilipili pia hufanya. Siku hizi Steve Nyerere naye
anafanya Stand Up Comedy.
Ni kwa kiasi gani Stand Up Comedy ya Steve inamuingizia hela ni jambo la
kujadili. Steve anaishi sababu ya jina lake kwa kufanya kazi za sanaa
au anaishi kisanii? Kuna uwezekano mkubwa pia kwamba licha ya sanaa,
Steve anaishi kisanii, ndiyo maana sanaa aliyosema aliitumia katika
kumuweka sawa mama Wema, inafanana sana na maisha yake halisi.
Steve anafika sehemu ambazo wengi hawawezi kufika na anazungumza na watu
ambao siyo kila msanii anaweza kuwafikia. Watu wote waliotajwa katika
ile sauti wanaweza kufikiwa na huyu msanii bila matatizo yoyote, ingawa
zipo pia chumvi za kutosha katika hilo.
Unashangaa kumuona Steve Nyerere akipanda katika jukwaa la muziki na
kuanza kumtunza mwimbaji manoti mengi mithili ya wale mapedeshee
tuliowazoea, kina Chief Kiumbe, Papaa Msofe, Muzamir Katunzi, Jack
Pemba, Ndama Mutoto ya Ng’ombe na wengine wa aina hiyo.
Kutoa ni moyo na si utajiri, lakini ni kweli kijana wa Kitanzania
anayepata hela kwa jasho lake kihalali, anaweza kugawa fedha nyingi
kwenye starehe kama Steve anavyofanya? Ingawa siungi mkono hata kidogo
kitendo kilichofanywa na Mama Wema, ni vyema nikamtahadharisha Steve
kwamba kilichotokea halikuwa jambo la bahati mbaya. Yale ndiyo maisha
yake, ya kutumia sanaa yake.
Na huenda siyo kwa mama Wema pekee, sanaa hiyo yaweza kuwa imetumika ‘kuwaweka’ sawa pia watu kibao ambao hatuwafahamu!
Tags
SIASA
