Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Serikali kupitia
vyombo vyake vya Dola kutoa sababu za kufuta jalada la uchunguzi wa Mkuu
wa Idara ya Sera na Utafiti wa chama hicho, Ben Saanane ambaye
ametoweka tangu Novemba mwaka jana.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema jana kwamba
jeshi hilo linafanya kazi yake huku akihoji, “Chadema wamejuaje kama
hilo jalada la kesi ya Saanane limefutwa?
“Nenda kawaulize tena, wao wamejuaje, wakueleze vizuri hilo jalada limefutwa vipi na nani?”
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene
ilisema wanashangazwa na hatua iliyofikiwa na vyombo vya dola kufuta
jalada la uchunguzi wakati kada huyo bado hajapatikana mpaka sasa.
“Tunajua DCI (Robert) Boaz alisema hawako naye lakini tunashangazwa na
hatua yao ya kufuta jalada la uchunguzi mapema bila hatua nyingine,”
inasomeka taarifa hiyo.
Hivi karibuni, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa
Mataifa (UN) yenye makao yake makuu jijini Geneva, Uswisi, ilisema iko
tayari kutuma timu ya uchunguzi.
Chadema imerejea kauli yake ya kuitaka Serikali kutoa maelezo ya wapi
alipo Saanane iwe ndani au nje ya nchi kwani ndiyo yenye udhibiti wa
mipaka yote majini, nchi kavu na angani.
Makene alisema Serikali ina teknolojia ya mawasiliano ya kuweza kujua na
kupata mawasiliano ya mwisho ya mtu aliyewasiliana na kada huyo, wakati
gani na juu ya suala gani.
Makene alisema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB),
imeshindwa kufanya kazi yake na kumaliza tofauti na sintofahamu
zinazoendelea.
Alisema ni aibu kwani taasisi za kimataifa zinaguswa na suala hilo huku vyombo vya usalama nchini vikikaa kimya.
Saanane, ambaye pia ni msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
alipotea katika mazingira ya kutatanisha Novemba 18 mwaka jana.
