BEKI wa pembeni wa Yanga, Juma Abdul amesema hataki kubishana na Mkuu wa
Kitengo cha Habari na Mawasiliani wa Simba, Haji Manara na badala yake
yeye atamuonyeshea kwa vitendo ndani ya uwanja.
Kessy aliitoa kauli hiyo mara baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara
iliyochezwa juzi Jumatano na Yanga kufanikiwa kuibuka kwa ushindi wa
mabao 2-0 huku beki huyo akianza kwenye kikosi cha kwanza cha Mzambia,
George Lwandamina.
Beki huyo, tangu atue kuichezea Yanga hakuwa na nafasi ya kucheza katika
kikosi cha kwanza cha timu hiyo na mara kadhaa amekuwa akitokea benchi
katika timu hiyo. Akizungumza na Championi Ijumaa, Kessy alisema aliiona
na kuisoma ‘post’ ya Manara kwenye ukurasa wake wa Instagram ambayo
ilikuwa ikimdhihaki kutokana na kukaa benchi.
Kessy alisema baada ya kuisoma hakutaka kumjibu na badala yake alikaa
kimya kuhofia majibizano yasiyokuwa na maana na badala yake akili zake
alizielekeza kwenye kucheza soka pekee. “Hivi vitu vinavyotokea hivi
sasa kutoka kwa viongozi wa Simba akiwemo huyo Manara nilivitarajia
tangu natoka Simba ninakuja kuichezea Yanga.
“Nakumbuka mwanzoni wakati nasaini kuichezea Yanga nilikuwa najibizana
nao kwenye vyombo vya habari, lakini baada ya kugundua kuwa ninatoka
mchezoni ninapojibizana nao, nikaamua kukaa kimya.
“Hivyo, sitaki kumkaribisha ibilisi hivi sasa na badala yake nitakaa
kimya nikifanya kazi yangu ndani ya uwanja kwa kuwajibu kuonyesha
kiwango kikubwa kwa lengo la kuipa ubingwa timu yangu ya Yanga,” alisema
Kessy.
Tags
MICHEZO KITAIFA
