Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa mwezi mmoja kwa
Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari kuwasilisha taarifa za
wanafunzi waliopata mimba pamoja na kuolewa wakiwa bado wanasoma.
Maelekezo hayo yametolewa jana
jijini Dar es Salaam na Waziri Ummy Mwalimu alipokuwa akizindua Ripoti
ya Utafiti wa Visababishi na Madhara ya Ndoa za Utotoni nchini Tanzania
uliofanywa kwa ushirikiano wa Wizara hiyo na Mashirika yasiyo ya
Kiserikali yakiwemo ya Plan International, Children’s Dignity Forum,
UNFPA, FORWARD pamoja na REPOA.
Alisema, wakati Sheria ya Ndoa
inafanyiwa marekebisho, wizara yake inatumia marekebisho ya Sheria ya
Elimu yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo
June 2016 ambayo yanakataza mtu yoyote kumuoa mtoto wa shule ya Msingi
au Sekondari kwani ni kosa la jinai lenye adhabu ya miaka 30 jela.
“Sheria hii inamtaka Mwalimu Mkuu
kuandaa taarifa ya kila robo mwaka kuhusu jumla ya watoto waliopata
ujauzito na kuolewa wakiwa bado wanasoma na taarifa hiyo kupelekwa kwa
Kamishna wa Elimu, lakini tangu sheria hiyo ianze kutumika hakuna
Mwalimu Mkuu aliyetii sheria hiyo hivyo natoa maelekezo kwa walimu hao
kukusanya taarifa hizo ndani ya mwezi mmoja,”alisema Waziri Ummy.
Ameongeza kuwa bila kuwapeleka wazazi na wahusika wa matukio hayo mahakamani na kufungwa tatizo hilo haliwezi kuisha nchini.
Aidha, Waziri Ummy amewataka
Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kila Halmashauri kupita nyumba kwa nyumba
kuwaibua wazazi wanaofanya vitendo hivyo na kuwasilisha taarifa hizo
sehemu husika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sheria hiyo.
Ametoa rai kwa Wadau wote wa
Maendeleo nchini kwenda zaidi Vijijini kuwasaidia wanawake na wasichana
waliopo huko kwani ndio maeneo yenye waathirika wengi wa matatizo ya
ndoa pamoja na mimba za utotoni.
Nae, Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi
wa Mtoto kutoka Shirika la Plan International – Tanzania, Jane Mrema
amesema, mnamo mwaka 2016 ripoti ya wasichana ilionyesha nafasi ya
watoto wa kike ulimwenguni haionekani kwa sababu takwimu zinazowahusu
ziko nyuma ya wakati, hazijakamilika na muda mwingine tafiti zake
hazifanyiwi utekelezaji.
“Nchini Tanzania hatuna takwimu
sahihi zinazoonyesha uhalisia wa changamoto anazozipata mtoto wa kike
kutokana na ndoa za utotoni na hiyo ndio sababu kubwa iliyopelekea
shirika letu kuungana na Serikali pamoja na mashirika mengine kufanya
utafiti huu ambao tumeuzindua rasmi leo,”alisema Bi. Jane.
Amefafanua kuwa shirika hilo
pamoja na Serikali ya Canada wamejitolea fedha kwa ajili ya kuandaa
vitabu vinavyoonyesha tafiti hizo katika lugha ya Kiswahili na
kiingereza ambavyo watavigawa mashuleni na mitaani ili kuweza kuwasaidia
watoto kupata uelewa na maarifa juu ya athari za ndoa hizo.
Shirika hilo linaendelea na
harakati za kupigania kumaliza tatizo hilo nchini ambapo kwa sasa
wamezindua Mpango Kazi wa miaka 5 unaoanza mwaka 2017- 2022 ukiwa na
lengo la kuwasaidia wasichana zaidi ya 1,000,000 ulimwenguni kote ambao
utawawezesha wasichana kujitambua, kujisimamia na kuhakikisha hakuna
anayeachwa nyuma katika suala zima la maendeleo.
Tags
AFYA