Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema mtu aliyemtishia kwa
bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape
Nnauye si askari wa Jeshi la Polisi, lakini ameshapatikana na
atashughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa ulinzi na usalama.
Mwigulu alisema hayo baada ya kufungua mkutano wa kazi wa mwaka wa
maofisa waandamizi wa polisi, makamanda wa mikoa na wakuu wa vikosi wa
Jeshi la Polisi ambao unafanyika mjini hapa. “Ameshapatikana
(aliyemtishia Nape) na atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za ulinzi
na usalama ambazo zimekuwa zikifanyika ndani, lakini
hazitangazwi,”alisema.
Hata hivyo, Mwigulu alikataa kuelezea kwa undani kuhusu mtu huyo kwa
kubainisha anatoka taasisi gani wala jina la mtuhumiwa kwa madai kuwa ni
kwa sababu ya usalama wake. Mtu huyo alifanya kitendo hicho wakati
Nape, ambaye alikuwa Waziri wa Habari, alipokuwa anaelekea Hoteli ya
Protea alikopanga kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mbunge huyo
wa Mtama kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.
Mtu huyo alikuwa pamoja na wenzake wawili ambao kwa pamoja walikuwa
wakimlazimisha arudi kwenye gari lake na kuondoka, lakini Nape alibisha
na ndipo mtu huyo aliporudi nyuma, kuchomoa bastola kutoka kiunoni na
kisha kumtishia kabla ya kutulizwa na mwenzake.
Watu hao walitoweka eneo hilo muda mfupi baadaye. Siku moja baada ya
tukio hilo Mwigulu alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu
kumtafuta mtu huyo.
