Ndizi ni miongoni mwa tunda lenye ladha nzuri na hupendwa na watu wengi
katika nchi mbalimbali hapa ulimwenguni ikiwemo Tanzania, ndizi ina aina
tatu za kipekee za sukari zinazojulikana kitaalam kama ‘sucrose’,
‘fructose’ na ‘glucose’ na vile vile ina kiasi kingi cha nyuzi yaani
'fiber' ambazo husaidia sana katika usagaji wa chakula tumboni.
Pia tunda hili linaelezwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuongeza na kuimarisha
nishati ya mwili, ambapo pindi ulapo tunda hili unaweza kupata nishati
ya kufanya kazi ya muda wa dakika 90 endapo utakuwa umekula ndizi mbili
tu na kwa sifa hiyo tunaweza kusema ndizi huenda likawa tunda muhimu
sana pia kwa wanamichezo.
Hata hivyo, nishati siyo faida pekee unayoweza kuipata katika ndizi
kwani pia ni tunda lenye uwezo wa kuponya na kuzuia matatizo mengine ya
kiafya likiwemo suala la mfadhaiko wa akili (depression)
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chama cha Afya ya Akili cha Taifa
(MINDI) cha nchini Uingereza kwa watu wanaosumbuliwa na tatizo la
mfadhaiko wa akili, watu wengi waliondokana na tatizo hilo na kujisikia
vizuri baada ya kula ndizi mbivu. Hali hii inatokana na ukweli kwamba
ndizi huwa na kirutubisho kinachojulikana kama ‘tryptophan,’ ambacho ni
aina fulani ya protini inayotumika mwilini kumfanya mtu kuwa mtulivu na
mwenye furaha.
Hali kadhalika, ndizi pia huwasaidia wanawake wanaopata matatizo wakati
wa hedhi, hivyo endapo wewe ni miongoni mwa wale akina mama wanaopatwa
na matatizo mbalimbali ya kiafya wakati wa hedhi, unashauriwa kula ndizi
mbivu na unaweza kuponywa.
Mbali na kusaidia wakina mama katika matatizo ya hedhi pia ndizi huweza
kuwasaidia watu ambao husumbuliwa na tatizo la upungufu wa damu
(anemia), hii ni kwasababu ndizi imekuwa ni chanzo kizuri cha madini ya
aina ya chuma (iron), hivyo inaweza kuwa ni dawa ya kuzuia na kuponya
tatizo la upungufu wa damu kwasababu madini ya chuma huamsha uzalishaji
wa chembechembe za damu mwilini.
Ama hakika tunda hili ni la kipekee kwani pia huweza kusaidia
kukabiliana na tatizo la shinikizo la damu kwani lina kiwango kikubwa
cha madini ya ‘potassium’ na wakati huo huo pia tunda hili lina kiasi
kidogo cha chumvi ‘sodium’ na hivyo kulifanya kuwa tunda bora katika
kupambana na tatizo la kupanda na kushuka kwa shinikizo la damu na
katika kuonesha uwezo wa tunda hili juu ya kusaidia kukabilina na
shinikizo la damu ni pale ambapo miaka ya hivi karibuni Mamlaka ya Dawa
na Chakula ya nchini Marekani iliamua kuwaruhusu wazalishaji na wauzaji
wakubwa wa ndizi nchini humo, kutangaza rasmi uwezo wa ndizi katika
kupambana na hatari ya shinikizo la damu na kupatwa na kiharusi (stroke)
kwa binadamu.
Lakini mbali na hayo pia hivi karibuni wanafunzi wapatao 200 katika
shule ya Twickenham nchini Uingereza, waliweza kufaulu mitihani yao kwa
kula chakula cha mchana, ambapo inaelezwa kuwa ndizi ziliongeza uwezo
wao wa kufikiri. Hii ni kwasababu utafiti unaonesha kuwa 'potassium'
inayopatikana kwa wingi katika ndizi inaaminika kuwa na uwezo wa
kumsaidia mwanafunzi kuamsha uwezo wake wa kufikiri zaidi.
Sambamba na faida hizo za tunda hili pia inaelezwa huweza kusaidia
kupunguza Kasumba yaani 'hangovers' ndizi ni moja ya dawa ya haraka ya
kuondoa uchovu unaotokana na ulevi wa jana yake (hangovers) , hivyo
unaweza kunywa ‘milk shake’ iliyotengenezwa kwa ndizi na kutiwa asali.
Ndizi hutuliza tumbo ikisaidiwa na asali, inayorejesha kiwango cha
sukari kilichopungua kwenye damu wakati maziwa nayo hutuliza na
kurejesha maji kwenye mfumo wake.
Pamoja na hayo ndizi pia husaidia katika matatizo mengi na kutuliza
mishipa ya fahamu, kuondoa wasi wasi, kutuliza vidonda vya tumbo,
tindikali na kushusha joto mwilini pamoja na kurekebisha mapigo ya moyo.
n.k.
Tags
AFYA
