MTOTO mwenye umri wa miaka minne amewashangaza wengi baada ya kuzungumza
kwa lugha saba kwa ufasaha katika kipindi cha televisheni nchini Urusi.
Video inamwonesha msichana huyo, Bella Devyatkina akionesha umahiri
wake kwa sasa inavuta watu kote duniani baada ya msichana huyo
kuzizungumza kiufasaha lugha hizo moja baada ya nyingine.
Msichana huyo mweye kipaji alishiriki katika kipindi hicho cha
televisheni cha Urusi cha 'Udivitelniye Lyudi' yaani ‘Watu wa Ajabu’
akiwashangaza majaji mjini Moscow kwa ujuzi wake huo wa lugha.
Mbali ya kufahamu vyema Kirusi, Bella pia anazungumza Kiingereza,
Kijerumani, Kihispania, Kifaransa, Kichina na Kiarabu kwa ufasaha; zote
hizo ni lugha zinazotambulika rasmi kwa matumizi katika Umoja wa
Mataifa.
Sehemu inayoshangaza zaidi ni kwamba Bella anaweza kuzungumza kwa
ufasaha katika lugha hizo, huku ujuzi wake ukizidi ule wa msamiati wa
mazungumzo rahisi ya kawaida.
Wakati wa kipindi aliweza kujibu maswali yaliyohusu mtaala wa shule kwa kutumia lugha hizo zote na hata kuimba nyimbo zao.
Mama wa Bella, Yulia anaeleza kuwa alianza kumfundisha bintiye huyo lugha hizo wakati alipokuwa na umri wa miaka miwili.
Walianza kwa somo la Kiingereza, lakini baadaye aliona kuwa Bella
alikuwa akifurahia somo na hivyo akaanza kuongeza lugha nyingine za
kumfundisha.
Bella alifanyia kazi lugha ya Kiingereza na mama yake huku lugha nyingine akifundishwa na wazungumzaji wa asili wa lugha hizo.
Kama ilivyotarajiwa wataalamu wa lugha wameshangazwa na uwezo wa Bella
kama ilivyokuwa kwa watazamanaji walioshuhudia kwa macho, kupitia
televisheni au kuiona video mtandaoni.
Mtaalamu mmoja wa lugha alikaririwa akisema: “kesi kama hizi ni nadra
mno lakini zimewahi kutokea huko nyuma. Lugha hujikita katika ubongo wa
mwanadamu na kuendelea katika hatua tofauti za maendeleo.”
Anaamini kuwa Bella hatapoteza ujuzi wake lakini alionya kwamba wakati
fulani unaweza kupotea iwapo hautafanyiwa kazi mara kwa mara kimazoezi.
Wakati akiendelea kujifunza lugha, dogo Bella anasema ndoto yake ni kuwa
nguva jike kama alivyo kipenzi chake Ariel wa picha ya vibonzo za
Disney– ambaye pengine ni moja ya sababu ya Bella kuwa na uwezo wa
kuzungumzia kiufasaha wanyama wa baharini.
Tags
MAAJABU
