Tanzania ina wanachama hai zaidi ya 600 wa kundi la watu wenye imani ya
siri ya Freemasons wakiwa wanatokana na watu wa kada mbalimbali wakiwemo
maarufu, huku ikielezwa kwamba miongoni mwao hakuna viongozi wakuu wa
serikali.
Hayo yalibainishwa na Kiongozi wa kundi la Freemasons katika eneo la
Afrika Mashariki, Jayantilal Keshavji Chande maarufu kama Sir Andy
Chande.
Kiongozi huyo Mtanzania mkazi wa Dar es Salaam mwenye asili ya Kiasia,
alisema licha ya Tanzania kuwa na wanachama hao, kwa sasa idadi ya
wanachama duniani inapungua tofauti na inavyoonekana sasa kuwa
wanaongezeka kutokana na kuibuka maneno mengi kuhusu kundi hilo.
Alisisitiza kuwa si rahisi kumjua mwanachama wa kundi hilo, bali wenyewe
ndio wanaofahamiana, akisema ni siri na kwamba wenyewe wanakutana
katika vikao mbalimbali mara moja kwa mwezi au zaidi.
Alisema nchini kuna wanachama zaidi ya 600 wakiwemo wafanyabiashara,
watumishi serikalini, walimu pamoja na wanataaluma mbalimbali
wanaoheshimika sana na kusisitiza kuwa kuna maneno mengi yanayosemwa
kuhusu kundi hilo, ambayo siyo ya kweli.
Alisema idadi ya wanachama wake duniani inazidi kupungua kutoka milioni
nane hadi sasa wako milioni sita, tofauti na wengi wanaodhani kuwa idadi
hiyo inaongezeka.
Chande alizungumza na mwandishi wa habari hizi katika Shule ya Sekondari
ya Shaaban Robert ambako yeye ni Mwenyekiti wa Bodi ya shule
alipozungumzia maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Alisema duniani kuna watu wazito wengi ambao ni wanachama wa kundi hilo
kama majaji wakubwa na hata Binamu wa Malkia Elizabeth wa Uingereza ni
kiongozi mkubwa wa kundi hilo.
Akizungumzia masharti ya kujiunga na kundi hilo, Chande alisema ni
lazima mwanachama huyo awe anaamini katika Mungu bila kubagua iwapo ni
Mkristo au Muislamu.
Alisema pia ni lazima anayetaka kujiunga awe na umri unaozidi miaka 21
na walio chini ya umri huo hawaruhusiwi kujiunga na lazima familia ya
anayetaka kujiunga na wanandugu wafahamu kuwa umejiunga na kundi hilo.
“Unajua katika imani hii kuna michango mbalimbali ambayo unatakiwa kutoa
ambayo ni zaidi ya dola milioni sita (karibu Sh bilioni 10), hivyo ni
lazima ndugu wafahamu ili kuepuka matatizo utakapotakiwa kutoa,”
alisisitiza.
Alisema si kweli kuwa wenye fedha wengi ni wanachama wa kundi hilo huku
akikanusha wanachama wanajiunga kwa ajili ya kupata fedha, bali ni dini
kama imani nyingine.
Alisisitiza kuwa hakuna ukweli kwamba wanaopata mafanikio katika maisha
wakiwa ndani ya imani ya Freemasons kuwa wanatoa kafara watu wao wa
karibu kwa lengo la kupata utajiri.
Chande pia alisema hairuhusiwi kutumia jina la kundi hilo kwa nia ya
kujipatia nafasi sehemu mbalimbali au kuongeza nafasi katika chuo au
shule.
Tags
Freemason