Mama mlezi wa aliyekuwa Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya
Kikwete, Bi Nuru binti Halfani Shomvi amefariki dunia katika Hospitali
ya Muhimbili alipokuwa akitibiwa asubuhi ya leo.
Kupitia mtandao wa twitter, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akishukuru jamii
kwa salamu za pole alizopokea amesema shughuli za msiba ziko nyumbani
kwa marehemu Mzee Kikwete, Mtaa wa Caravan, Bagamoyo na maziko yatakuwa
Bagamoyo mjini, kesho Jumatano Machi 8, 2017 saa 10 Alasiri.
"Mama amefariki jana usiku saa nane, akiwa na miaka 91. Baba yangu, Mzee
Halfani Mrisho Kikwete alikuwa na wake wawili alipofariki 1998. Mama
yangu mzazi Bi Asha binti Jakaya, aliyekuwa mke mkubwa wa Mzee Halfani
Kikwete alifariki 1999; tukabaki na mama yetu huyu mdogo". Kauli ya
Jakaya Kikwete
Naye Mbunge wa Chalinze Mhe. Ridhiwan Kikwete ambaye ni mjukuu wa
marehemu ndiye aliyekuwa wa kwanza kuthibitisha kutokea kwa kifo hicho
asubuhi ya leo.
"Ndugu na marafiki nasikitika kuwatangazia msiba/kifo cha Bibi yetu Bi.
Nuru Khalfan Kikwete kilichotokea asubuhi hii katika Hospitali ya
Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa matibabu. Taratibu za mazishi
tutajulishana" Amesema Ridhiwan Kikwete.
Tags
TANZIA

