Serikali imefuta usajili wa vibali vya uzalishaji na Uingizaji wa aina
20 ya pombe kali za viroba zilizokuwa zimesajiliwa na Mamlaka ya Chakula
na Dawa (TFDA).
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu
ameyasema hayo leo, Jijini Dar es Salaam kuhusu usitishaji wa uzalishaji
na uingizaji, uuzaji na matumizi ya pombe zilizofungwa katika mifuko ya
plastiki (Viroba).
“Tumefuta usajili wa vibali vya uzalishaji na uingizaji kutoka nje,
usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zilizofungashwa katika
mifuko ya plastiki (viroba) chini ya ujazo wa milimita 200,” alifafanua
Ummy Mwalimu.
Aliendelea kwa kusema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa tamko la Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa alilotoa Februari 02, 2017 la kusitisha uzalishaji,
uingizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe hiyo kali kuanzia
Machi 01, 2017.
Ummy amesema kuwa usitishaji huo unazingatia kanuni za kukataza
uzalishaji, uingizaji na matumizi ya vifungashio vya plastiki
kufungashia pombe kali za mwaka 2017 (The Environmental Management
(Prohibition of Manufacturing, Important and Use of Plastic Sachets for
Packakging Distilled and other alcoholic beverages) Regulations 2017)
imekatazwa kutumia vifungashio vya plastiki kufungashia pombe kali.
Badala yake wazalishaji watapaswa kufungasha pombe kali hizo katika
chupa zenye ujazo usiopungua mililita 200.
Aidha amesema kuwa uamuzi wa kupiga marufuku matumizi ya pombe za aina
hiyo unatokana na athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kiafya na
kijamii. Matumizi mabaya ya pombe hizo yamesababisha ajali nyingi, vifo,
ulemavu na mzigo mkubwa kwa Serikali wa kutoa huduma kwa wahanga wa
pombe hizo na ongezeko la makosa ya jinai.
Ummy amesema kwamba Viroba vilivyokamatwa na kuzuiwa vinasubiri maelekezo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu namna ya kuviteketeza.
Tags
POMBE ZA VIROBA
