Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) inatararajia kuanza upasuaji wa kupandikiza Moyo kwa wagonjwa
wenye matatizo ya moyo nchini.
Mkurugenzi wa Upasuaji na Daktari
Bingwa wa Upasuaji wa Moyo na Mishipa ya Damu Dkt. Bashir Nyangasa
ameyasema hayo leo Jijini, Dar es Salaam alipokuwa akiongea na vyombo
vya habari kuhusu malengo ya Taasisi hiyo.
“Tuko katika maandalizi ya kuandaa
mapendekezo kwa ajili ya kupeleka Bungeni ili Bunge lilidhie na
kupitisha sheria itakayoruhusu mtu kuandika wosia wa viungo vyake
kutumika mara baada ya kufariki, ikiwemo moyo, figo na viungo vingine,”
alifafanua Dkt. Nyangasa.
Aliendelea kwa kusema kuwa,
umefika wakati kwa watanzania kujiwekea utaratibu wa kuacha wosia wa
kutumika kwa viungo vyao mara baada ya kufariki kwa ajili ya kuhifadhiwa
katika benki za viungo ili viweze kutumika na watu ambao wanauhitaji.
Aidha Dkt. Nyangasa amesema
hospitali ya Apolo Bangalole ya India na hospitali nyingine za kimataifa
za magonjwa ya moyo kwa sasa zimehamia JKCI kutokana na huduma pamoja
na vifaa vinavyopatikana katika hospitali hizo vinapatikana katika
Taasisi hiyo.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi
Huduma za Tiba, Daktari Bingwa wa Wagonjwa wa Moyo Dkt. Tulizo Shemu
amesema kwa mwaka 2016 Taasisi imefanya uchunguzi wa tiba kwa wagonjwa
973, kati ya wagonjwa hao 620 walipatiwa matibabu ya moyo ya bila
kufungua kifua kwa kupitia mishipa ya damu (Catheterization) na wagonjwa
353 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua.
Vilevile amesema kuwa kwa mwaka
huu wa 2017 Taasisi hiyo imejipanga kufanya upasuaji wa kupasua kifua
kwa wagonjwa 700 na wagonjwa wengine 1000 watafanyiwa operesheni bila
ya kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa ‘Catheterization’.
Taasisi hiyo inategemea kuwa na
kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Open
Heart International ya nchini Australia kuanzia Machi 10, 2017 ambapo
wagonjwa 25 wakiwemo watoto 15 na watu wazima 10 watafanyiwa upasuaji.
Wananchi wameombwa kujitokeza kuchangia damu kutokana na uhitaji wa damu nyingi katika upasuaji huo.
Tags
AFYA