Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
leo tarehe 16 Machi, 2017 ametembelea eneo la ujenzi wa Ikulu Chamwino
Mkoani Dodoma na kuwahakikishia wananchi kuwa atahamia Dodoma hivi
karibuni kama alivyoahidi.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenister Joakim Mhagama na
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema pamoja na majengo ya
Ikulu Serikali itajenga miundombinu mingine zikiwemo reli na barabara za
lami zitakazounganisha maeneo ya vijiji vinavyozunguka Ikulu na mji wa
Serikali.
Pia Mhe. Dkt. Magufuli amewahakikishia wananchi kuwa wote watakaoguswa
na shughuli za ujenzi wa miundombinu ya Serikali na wanaostahili kulipwa
fidia watalipwa, na ametoa wito kwa wananchi hao kutumia fedha za fidia
watakazolipwa kujenga makazi bora na kujipanga kufanya shughuli zenye
manufaa kwao.
“Hapa sasa watakuja watu wengi, wafanyakazi na wageni maana tayari
Mabalozi wa nchi mbalimbali nao watajenga ofisi zao hapa, sasa na nyinyi
mjipange kufanya biashara, mtapata soko la kuuza mazao na bidhaa
nyingine, mkipata fedha ziwasaidie kwa manufaa na sio kuzichezea”
amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema
utekelezaji wa Serikali kuhamia Dodoma unakwenda vizuri ambapo mpaka
sasa viongozi wakuu wa wizara zote na wafanyakazi 2,069 wameshahamia
Dodoma na wengine wanaendelea kuhamia Dodoma.
Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa atasimamia utekelezaji wa maagizo ya Mhe.
Rais Magufuli aliyeagiza kujengwa kwa reli itakayounganisha eneo la
Bwigili na Dodoma mjini ili kurahisisha usafiri wa watu pamoja na
kuharakisha ujenzi wa barabara za kuzunguka mji wa Dodoma na barabara za
kuunganisha mji wa Serikali na Dodoma Mjini.
Wakiwa katika eneo hilo, Mhe. Rais Magufuli na Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa
wameshiriki ufyatuaji wa matofari yatakayotumia katika ujenzi wa
majengo ya Ikulu.
Mapema kabla ya kutembelea eneo hilo, Mhe. Rais Magufuli amepokea
taarifa ya mapendekezo ya ujenzi wa Mji wa Serikali wa Makao Makuu
Dodoma kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu
Mhandisi Paskasi Muragili na kuagiza ujenzi wa Mji huo uzingatie maslai
ya Taifa.
Tags
RAIS MAGUFULI
