Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi amewaagiza makatibu wakuu wote
wa wizara kuhakikisha wanakuwapo Dodoma wakati wote na wakienda Dar es
Salaam iwe ni kwa shughuli maalumu.
Balozi Kijazi aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na makatibu wakuu hao kwenye kikao cha kikazi.
Alisema japokuwa bado kuna watumishi wamebakia Dar es Salaam, lakini wao
wanatakiwa kujipanga kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa ufanisi
katika miji yote miwili. Alisema wizara zote hadi jana zilikuwa
zimeshahamia mkoani Dodoma.
“Niwatake makatibu wakuu muwepo Dodoma muda wote na si kuchungulia tu,
tuwepo hapa. Mtakuja Dar es Salaam kama kuna majukumu muhimu tu,”
alisema Balozi Kijazi.
Alisema amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu kuandaa taarifa
ambayo ataiwasilisha katika Baraza la Mawaziri ili litoe uamuzi ni wapi
mji huo wa kiserikali utajengwa.
Alisema hivi sasa watakuwa katika majengo ya muda, wakati suala la kuwa
na mji wa Serikali (government city) likiendelea kuzungumzwa.
Balozi Kijazi alisema kila wizara itaendelea kutumia majengo
waliyopangiwa, wakati wakijipanga kujenga yao katika mji wa kiserikali.
Tags
HABARI KITAIFA
