Mtafiti wa viumbe hai na mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Bayreuth cha
nchini Ujerumani, Dk Andrew Hemp ameelezea sifa za mti ujulikanao kama
Mkukusu kuwa unaweza kuishi kati ya miaka 200 hadi 300, lakini
ulioonekana nchini una miaka 600.
Akiuzungumzia mti huo ambao unapatikana katika Kijiji cha Tema wilayani
Moshi, mtafiti huyo amesema mti huo ambao ni mrefu kuliko yote barani
Afrika una urefu wa mita 81.5 na uko katika eneo lililopo kwenye Hifadhi
ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa).
Dk Andrew amesema kwa mujibu wa utafiti mti huo una uwezo wa kuishi miaka hiyo kwa kutunzwa na kuhifadhiwa.
Amesema kwamba katika utafiti walioufanya barani Afrika waligundua miti
mirefu 31, lakini Mkukusu wa Moshi ndiyo mrefu kuliko yote na una umri
wa miaka 600 hivi sasa ukiwa umevuka kiwango cha juu cha maisha ya miti
ya aina hiyo.
Tayari Serikali imeiagiza Kinapa kuboresha miundombinu ya barabara ili
kuweza kuufikia mti huo iwapo watalii watataka kwenda kuuona.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki amesema mti huo utasaidia
kuongeza mapato kwa kasi kwa kuwa ni kivutio kipya cha utalii ndani ya
mkoa huu.
Tags
UTAFITI
