UKAIDI! Wakati wakazi mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji
vyake wakiendelea kutii bila shuruti agizo la kuacha kunywa pombe,
kucheza pool na kamari nyakati za kazi, baadhi ya vijana wakaidi
wameonekana kupuuza agizo hilo linalotafsiriwa kama kumchezea sharubu
Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda aliyetoa amri hiyo.
Uchunguzi mahususi uliofanywa na Kitengo Maalum cha Oparesheni Fichua
Maovu (OFM) cha Global Publishers kimefichua kuendelea kwa michezo ya
pool, uchezeshwaji wa kamari na unywaji pombe katika baadhi ya baa na
maeneo maarufu, tena vitendo hivyo vikifanyika mchana kweupe.
Katika uchunguzi huo uliofanywa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kama
Sinza, Manzese, Temeke, Mbagala na Kariakoo, OFM walishuhudia majira ya
kuanzia saa nne asubuhi, katika baa kadhaa, wahudumu wakiendelea na
utoaji wa huduma za vilevi bila wasiwasi wowote. Sinza Mori katika baa
moja maarufu, ilishuhudiwa baadhi ya watu katika bar hiyo wakiendelea
kunywa bia kama kawaida kana kwamba bado wanaishi enzi zile za mwaka
1947.
Kule Manzese, katika baa moja kubwa yenye wateja wengi (majina yao
yanahifadhiwa kwa sasa) baadhi ya wateja waliwekwa sehemu ambayo siyo
rahisi kuonekana na mtu mgeni, huku wahudumu wakiwapelekea vilevi vyao.
OFM ilikuta wanywaji wakipewa bia, pombe kali za kwenye chupa na virobo
ambavyo vimepigwa marufuku. Temeke Mwembeyanga, katika baa maarufu eneo
hilo, OFM pia walikuta agizo la Mheshimiwa Makonda likipuuzwa mchana wa
jua kali, kwani watu waliendelea kupata kile roho inapenda bila hofu
yoyote.
Licha ya unywaji wa pombe, pia katika eneo la Mbagala Rangi Tatu, OFM
iliwaona baadhi ya vijana wakiendelea na mchezo wa pool bila hofu, licha
ya kuwa jua lilikuwa likiwaka, kuashiria muda wa watu kuchapakazi.
Lakini katika hali ya kusikitisha, eneo la katikati ya Kariakoo, kwenye
baa moja kubwa ya miaka mingi, pamoja na jua kali la mchana, uuzwaji na
unywaji wa pombe ulikuwa ukifanyika pasipo kificho, huku vijana wa rika
mbalimbali nao wakionekana wacheza pool, katika meza zaidi ya nne
zilizomo ndani ukumbi wa baa hiyo.
Licha ya mitungi, pia baadhi ya wateja waliendelea kucheza kamari ya
kwenye vibanda maarufu kama casino pasipo hofu licha ya kwamba baa hiyo
ipo umbali wa mita chache tu kutoka kilipo Kituo cha Polisi cha
Msimbazi, jijini Dar es Salaam. Licha ya Makonda kutoa amri ya kuachwa
kwa vitendo hivyo wakati wa saa za kazi, pia viongozi wengine wa ngazi
za ukuu wa wilaya, mikoa na mawaziri, wamewahi kutoa maagizo ya
kutochezwa kwa pool, kunywa pombe na hata kwa wamiliki wa maeneo
yanayoendesha shughuli hizo kufungwa nyakati za kazi.
Tags
Paul Makonda
