Viwanja vya Nyerere Square mjini
Dodoma mahali ambapo kunafanyika sherehe za kuwapokea viongozi
mbalimbali wa serikali baada ya kuhamia Dodoma.
…………………………………………………………….
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla maalumu ya
kuwakaribisha viongozi wa Serikali itakayofanyika Machi 5 mwaka huu
mkoani Dodoma.
Hafla hiyo imeandaliwa na Uongozi
wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma na itafanyika mkoani humo katika viwanja
vya Nyerere (Nyerere Square) kuanzia saa 8 kamili mchana.
Afisa Habari wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa Dodoma, Jeremia Mwakyoma ameyasema hayo leo mjini Dodoma alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya ujio wa viongozi
hao katika Mkoa huo.
Mwakyoma amesema viongozi wa
Serikali kuhamia katika Makao Makuu ya Nchi ni sehemu ya utekelezaji wa
azma ya Serikali ya Awamu ya Tano hivyo Mkoa utawakaribisha rasmi
Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wa
Wizara waliohamia kutoka Jijini Dar es Salaam.
“Tukio la viongozi wa Wizara
kuhamia Makao Makuu Dodoma ni la kihistoria ndio maana uongozi wa
Serikali ya Mkoa umeona ni vema kuweka utaratibu rasmi wa kuwakaribisha
viongozi hao,”alisema Mwakyoma.
Afisa Habari Mwakyoma amewakaribisha wananchi wote wa Mkoa huo pamoja na Mikoa ya jirani kuhudhuria kwa wingi kwenye hafla hiyo.
Mnamo Julai 25 mwaka 2016 katika
maadhimisho ya siku ya mashujaa yalioadhimishwa mkoani Dodoma, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli alitangaza
rasmi Serikali kuanza mchakato wa kuhamia Dodoma ambapo ndipo yalipo
Makao Makuu ya Nchi.
Tags
SIASA