WAKATI mwili wa bilionea na mfanyabiashara maarufu wa vinywaji Festo
Mselia (58), ukitarajiwa kuzikwa kesho katika kijiji cha Umbwe Unana
mkoani Kilimanjaro, mambo mapya yameibuka kuhusiana na kifo chake
kinachodaiwa kutokana na kujipiga risasi.
Mambo mapya yaliyoibuka yakihusishwa na chanzo cha kifo hicho ni pamoja
na usumbufu alioupata polisi, kutuma ujumbe wa kumuaga mkewe na kumpigia
simu mdogo wake mara tisa bila kupokewa muda mfupi kabla ya umauti
kumfika.
Akizungumza na Nipashe jana, mdogo wa marehemu huyo, Anthony Mselia
alisema mwili wa marehemu baada ya kufanyiwa uchunguzi, umekutwa na
matundu matatu ya risasi kwenye maeneo ya chini ya kidevu.
"Mazingira yanaonyeshwa kwamba 'brother' (kaka) hajauliwa na mtu, yaani sielewi ni kitu gani kilichomsibu," alisema.
"Lakini kulikuwa na taharuki kuhusu suala la pombe kali aina za viroba,
lakini hakuna kitu alichowahi kuniambia zaidi ya kulalamikia suala hilo.
"Tangu siku ya kwanza alipokamatwa Machi 3, mwaka huu, alinipigia simu
na kuniambia kwamba serikali haioni namna yeyote ya kuongeza muda na hii
ilitokana na kwamba alikuwa na mzigo mkubwa wa bidhaa hiyo katika stoo
zake zaidi ya tatu tofauti wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni moja na
viroba ndio vilivyokuwa na mzunguko mkubwa wa biashara na ndivyo
vilikuwa vimekamata fedha."
Akisimulia zaidi, mdogo huyo wa marehemu alisema kaka yake aliwapeleka polisi zaidi ya stoo tatu.
Alisema kuwa kabla kaka yake hajafikia uamuzi huo Machi 7, yeye alifika nyumbani kwake na kumuaga kuwa anasafiri kwenda Moshi.
"Nilimsalimia na kumuaga kwa safari na akaniruhusu kuondoka na
hakuonekana kuwa na mawazo wala kitu chochote alikuwa 'happy' (na
furaha) tu. Nakumbuka aliniambia kwamba mdogo wangu ukienda uwahi kurudi
kutoka Moshi kwa kuwa mimi naishi hapa hapa Dodoma," alisema.
Aliendelea kueleza kuwa anaamini kaka yake hajafikia uamuzi huo kutokana
na kuwa na madeni aliyokuwa nayo ambayo alidai alikuwa ameshayalipa kwa
kiasi kikubwa.
"Kwa mfanyabiashara mkubwa kama Mselia ambaye ana mzunguko mkubwa wa
biashara, lazima kutakuwa na watu wanaoleta mizigo lakini siyo kesi ya
yeye kufikia hatua hiyo, mimi mpaka sasa hivi akili na aliponipigia simu
na kulalamika kilichompelekea kufanya uamuzi ni suala la viroba."
Alieleza kuwa awali polisi, maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) walifika dukani kwa kaka yake kumhoji
na kumkagua na kwamba marehemu alitoa ushirikiano na kuwapeleka kwenye
stoo zake na kuwaonyesha mzigo wote ambao alizuiwa kuuuza.
Alisema kuwa maofisa hao baada ya kumaliza kukagua, waliweka stika
lakini alikuwa bado analalamika kwanini mzigo wenye thamani kubwa ya
fedha ufungiwe ndani, jambo ambalo lilikuwa linampa wakati mgumu.
Alisema mzigo huo licha ya kuzuiwa kuuzwa, bado umo kwenye stoo zake.
SIMU MARA TISA
Mdogo huyo wa marehemu aliendelea kusimulia kuwa baada ya kuagana na
kaka yake, hakuwasiliana naye lakini baada ya kufika Moshi na kutaka
kumjulisha kwamba amefika salama, alibaini kuwa kaka yake alikuwa
amempigia simu mara tisa bila kumpokea.
"Muda mfupi baadaye nilipigiwa simu na polisi kwa namba zilizoishia 71 akiuliza kwamba 'wewe unamfahamu Mselia?',
nikamwambia ni kaka yangu, akaniambia mimi ni askari, kaka yako
amejipiga risasi, nikamuuliza amejipiga au imemfyatukia bahati mbaya?
"Akasema amejipiga mwenyewe, tafuta watu waende ‘General Hospital’ (Hospitali ya Rufaa ya Mkoa) kwa ajili ya kumpa msaada."
Alibainisha kuwa baada ya taarifa hiyo, alimpigia mke wa marehemu na
baadaye wakawapigia marafiki wa karibu wa familia na wakaungana naye,
lakini muda mfupi baadaye akapigiwa simu kuwa kaka yake amefariki.
Alidai kuwa marehemu alikuwa anamshirikisha matatizo yote ya kibiashara.
KWAHERI
Mdogo huyo wa marehemu pia alidai kuwa kaka yake alitumia ujumbe mfupi
wa maandishi kwa mkewe uliosomeka "kwaheri" muda mfupi kabla ya tukio la
risasi, lakini mke wake hakuutilia maanani akidhani alikosea kuutuma
kwake badala yake alikuwa anamuaga mtu mwingine.
"Lakini baadaye, baada ya kupata taarifa kuwa amejipiga risasi, aligundua kuwa kumbe alikuwa anamuaga," alisema Mselia.
"Kinachoonekana ni 'harrasment' ya polisi kwa sababu polisi walifika
mara ya kwanza, ya pili na ya tatu, Mselia wa watu maskini hapendi
kusumbuliwa."
KAULI YA POLISI
Akizungumza kwa simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro
Mambosasa, alidai maganda ya risasi yaliyokutwa pembeni ya mwa mwili wa
marehemu yalitumiwa na marehemu wakati akijaribu kujiua.
“Maganda yale ya risasi aliyatumia kujipiga mwenyewe, unajua alipokuwa
akijipiga nadhani hakujilenga vizuri na hii ni kutokana na kupaniki,
alijipiga kwenye shigo ikatokea mdomoni, hakufa na yeye alitaka afe sasa
kutokana na kujipiga kule alijipiga risasi tano," alidai Kamanda
Mambosasa.
Mfanyabiashara huyo alijiua juzi shambani kwake Msalato Manispaa ya
Dodoma baada ya kuhojiwa na polisi kuhusu shehena ya viroba aliyokuwa
nayo yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni moja.
Tags
POMBE ZA VIROBA
