SHIRIKISHO la Soka Rwanda (FERWAFA) limeteua Mjerumani Antoine Hey kuwa
kocha wake mpya wa timu ya taifa kwa mkataba wa miaka miwili.
Hey amepiku Raoul Savoy wa Uswisi na Rui Aguas wa Ureno, alioingia nao
fainali ya orodha ya mwisho ya watu watatu kuwania kurithi mikoba ya
Johnny McKinstry aliyeacha kazi Agosti mwaka jana.
“Kwa Hey, nafikiri tumefanya uteuzi mzuri, hususan tukizingatia tuna
uhusiano na Ujerumani,” amesema Rais wa FERWAFA, Vincent Nzamwita.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 46 anatarajiwa kutambulishwa siku chache
zijazo. Hey ana uzoefu na soka ya Afrika kwa ngazi ya timu za taifa na
hata klabu, kwani amewahi kufundisha Lesotho kati ya mwaka 2004 na 2006
kabla ya kuhamia Gambia na baadaye klabu ya US Monastir ya Tunisia mwaka
2007.
Pia amefanya kazi Liberia, Kenya na hivi karibuni El-Merreikh ya Sudan.
Anaingia katika orodha ya makocha wa Kijerumani waliofanya kazi Amavubi,
wengine wakiwa ni Otto Pfister aliyefundisha 1972 hadi 1976, Rudi
Gutendorf kuanzia 1999 hadi 2000 na Michael Nees aliyepiga kazi 2006
hadi 2007.
Ikumbukwe Rwanda itamenyana na Tanzania, Taifa Stars katika kuwania
tiketi ya Fainali za Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN)
mwaka 2018 nchini Kenya.
Hiyo ni itakuwa katika Raundi ya pili ya mchujo wa michuano hiyo
inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee na Taifa
Stars itaanzia nyumbani Dar es Salaam Julai 14, 15 na 16 mwaka huu kabla
ya kuwafuata Amavubi Kigali kati ya Julai 21, 22 na 23.
Mshindi wa jumla atamenyana na mshindi kati ya Uganda na ama Sudan
Kusini au Somalia katika Raundi ya Tatu ya mchujo mechi ya kwanza
ikichezwa kati ya Agosti 11, 12 na 13 na marudiano kati ya Agosti 18, 19
na 20, mwaka huu.
Tags
MICHEZO KIMATAIFA
