Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania
Jenerali Venance Mabeyo amefanya ziara ya kikazi Mkoani Kagera kukagua
maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kabyaile Wilayani Missenyi
kinachojengwa upya na Jeshi la Wananchi Tanzania mara baada ya
kuathiriwa na Tetemeko la Ardhi lililotokea Mwezi Septemba mwaka jana.
Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo
alifanya ziara hiyo Machi 2, 2017 na lengo kuu ilikuwa ni kuona
maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho mara baada muda alioutoa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kuisha mwishoni
mwa mwezi Februari mwaka huu 2017.
Rais Magufuli alipofanya ziara
Mkoani Kagera Januari 1, 2017 alitembelea eneo la Kabyaile Wilayani
Missenyi na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha afya na
kuagiza kuwa ujenzi huo uwe umekamilika ifikapo Mwisho mwa mwezi
Februari 2017.
Mara baada ya kukagua maendeleo ya
ujenzi huo Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo akiongea na viongozi wa mkoa
na wananchi waliofika kumuona kituoni hapo alisema ameridhishwa na
hatua iliyofikiwa katika ujenzi huo, pia alishukuru upanuzi wa majengo
kuwa ni manufaa kwa wananchi wa Kabyaile na Wilaya ya Missenyi kwa
ujumla.
Pia aliwashukuru wananchi kwa
ushirikiano wao na kikosi cha Jeshi la Wananchi Tanzania kinachojenga
kituo hicho kuwa kikosi hicho kinafanya kazi katika hali ya utulivu na
amani na wananchi wenyeji, aidha aliwaomba wananchi kuwaona wananjeshi
kama raia wengine na kuendelea kuwapa ushirikiano kwani wanatokana na
Watanzania wenyewe.
Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo
baada ya kukagua ujenzi na kupata maelezo ya kina alisema kuwa muda
alioutoa Rais Magufuli wa hadi mwishoni mwa Mwezi Februari 2017 ujenzi
haukuweza kukamilika kwasababu kuna kazi zingine za ziada ambazo
zilijitokeza na kushindwa kukamilisha kituo hicho kwa muda uliotolewa.
?Kwa kazi alizoelekeza Rais
Magufuli tayari zipo katika hatua za mwisho kabisa za umaliziaji, pia na
kazi zilizoongezeka zipo katika hatua nzuri ya ujenzi na kufikia
mwishoni mwa mwezi Machi 2017 kazi zote zitakuwa zimekamilika zote?
Aliwaeleza wananchi Mkuu wa Majeshi Jenerali Mabeyo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa
Majeshi ya Tanzania Jenerali Mabeyo alitembelea pia ujenzi wa Shule ya
Sekondari Omumwani Katika Manispaa ya Bukoba kunakojengwa vyumba viwili
vya mabweni na Kikosi cha Jeshi la Wananchi Tanzania, aidha alimalizia
ziara yake katika Shule ya Sekondari Ihungo na kukagua ujenzi mpya wa
shule hiyo iliyoharibiwa na tetemeko pia mwezi Septemba Mwaka jana 2016.
Tags
AFYA