RAIS Robert Mugabe wa Zimbabwe mwishoni mwa wiki iliyopita amefuja zaidi
ya dola milioni moja za Marekani kwa ajili ya kukodi ndege ya kifahari
Boeing 767-200 aliyoitumia kusafari katika nchi za Singapore na Ghana
ilihali nchi yake ikikabiliwa na uchumi mgumu kupindukia.
Hali ya kiuchumi nchini Zimbabwe inaripotiwa kuwa mbaya kiasi kwamba
imekuwa vigumu kulipa hata mishahara ya watumishi wa serikali.
Kwa mujibu wa Jarida la Indipendent, uchunguzi unabainisha kwamba ndege
hiyo aliyotumia Rais Mugabe, 767 Boeing Business Jet (BBJ) yenye usajili
P4-CLA, kuanzia Machi Mosi hadi Machi 6, mwaka huu, ilifanyiwa malipo
katika kampuni yake ya zaidi ya dola za Marekani milioni moja. Ndege
hiyo inaendeshwa na Kampuni ya Comlux Aviation, yenye ofisi zake
Bahrain.
Inaelezwa kwamba ndege hiyo ya kifahari inavyo vyumba vya faragha, ofisi
kubwa sambamba na muundo wa kuvutia ndani unaonakshiwa na vifaa vya
kisasa.
Taarifa hizi za Mugabe kukodi ndege ya kifahari kwa fedha nyingi
zinajitokeza huku tayari kukiwa kumeripotiwa taarifa nyingine
zinazobainisha kwamba kiongozi huyo huyo amekuwa na matumizi ya ufujaji
wa fedha katika usafiri.
Inadaiwa kwamba safari zake za ndani na nje ya nchi zimepata kutumia
takriban dola za Marekani milioni 36 katika miezi 10 ya mwanzo ya mwaka
2016 katika nchi ambayo sekta ya afya imekuwa ikikabiliwa na uhaba
mkubwa wa dawa, zikiwamo hata dawa za kutuliza maumivu katika hospitali
za umma.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya Jarida la Independent, Mugabe
amelazimika kukodi ndege hiyo ya kifahari baada ya ndege yake ambayo
amekuwa akiitumia kwa safari zake ya Shirika la Ndege la Zimbabwe
(AirZim) kuhitaji matengenezo makubwa kabla ya kuruka safari za masafa
marefu.
Hata hivyo, hali hiyo ya Shirika la Ndege la Zimbabwe kushindwa
kuifanyia matengenezo ndege hiyo kutokana na ukata inamweka katika
wakati mgumu mkwe wa Rais huyo wa Zimbabwe, Simba Chikore, ambaye ndiye
bosi mkuu wa operesheni katika shirika hilo la ndege la taifa.
AirZim, ambalo wakati Zimbabwe inapata uhuru mwaka 1980 chini ya Robert
Mugabe lilikuwa na jumla ya ndege 18 zilizokuwa zikifanya kazi, kwa sasa
shirika hilo limekuwa na jumla ya ndege nne tu zinazofanya kazi ambazo
ni Airbus A320, Boeing 767 na nyingine 737 pamoja na MA60 kutoka China.
“Shirika la Ndege la Zimbabwe limeshindwa kuifanyia matengenezo
yanayohitajika ndege ya Rais Mugabe kwa kuwa wakala wake wa vifaa bado
hajalipwa deni lake la awali,” kilieleza chanzo cha habari cha
Independent na kuongeza kuwa: “..shirika kwa sasa limekuwa katika hali
mbaya.”
Waziri wa Usafiri wa Zimbabwe, Joram Gumbo, aliliambia gazeti la
Independent mwishoni mwa wiki hii kwamba wizara yake imechukua uamuzi wa
kukodi ndege hiyo kwa kuwa ile inayotumiwa na Mugabe ya Shirika la
Ndege Zimbabwe ni mbovu.
“Tumelazimika kukodi ndege kutoka Bahrain kwa sababu ile ndege
inayotumiwa na rais inaendelea kufanyiwa matengenezo. Hivi
tunavyozungumza tayari vifaa kwa ajili ya matengenezo vimekwishaletwa na
muda si mrefu itakuwa hewani ikiendelea na shughuli, lakini rais
asingeweza kusubiri hadi matengenezo yakamilike ilipaswa aendelee na
ratiba yake,” alisema Gumbo na kuongeza; “Tulifanya jitihada za kutafuta
ndege ya kukodi katika ukanda wetu wa Afrika. Afrika Kusini nao
wamekuwa na matatizo yao kama ilivyo kwa Angola. Kukodi ndege kwa ajili
ya rais si jambo jipya na la ajabu, rais ndiye mteja namba moja wa
shirika letu.”
Kwa mujibu wa Gumbo, gharama za kukodi ndege hiyo ni za kawaida na
kwamba tofauti kubwa ya bei imetokana na ukweli kwamba ndege hiyo
imesafiri kutoka mbali.
Mugabe mwenye umri wa miaka 93, amesafiri kwenda Singapore kwa ajili ya
kutazamwa afya yake katika moja ya hospitali zenye gharama za juu kabisa
za matibabu nchini humo ya Gleneagles. Baada ya hapo, Mugabe atasafiri
kuelekea Ghana ambako atakuwa na ziara nchini humo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Kampuni ya Ndege ya Comlux, ndege ya aina hiyo,
yaani Boeing 767 BBJ imetengenezwa kwa ajili ya kutumiwa na marais wa
nchi mbalimbali, familia za kifalme na watu wengine mashuhuri katika
tasnia ya biashara duniani, ni ndege ya kifahari yenye uwezo wa kuchukua
abiria 63 ikisafiri kwa muda wa saa zaidi ya 14 angani bila kutua.
Uchunguzi zaidi wa gazeti la Independent unabainisha kwamba fedha
zilizotumika kukodi ndege hiyo zinajumuisha huduma zote zikiwamo za
chakula na vinywaji vya aina mbalimbali ikiwamo mvinyo, huduma ya simu
kwa njia ya Satellite na bima ya usalama.
“Kwa namna ndege hii ilivyo, inaonekana kuirusha kwa saa moja angani
inatumia dola za Marekani takriban 9,138,” anaeleza mtaalamu mmoja wa
masuala ya anga.
Katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016, Mugabe alisafiri umbali wa
kilomita 200,000 angani. Akiwa amesafiri kwenda nchini Singapore zaidi
ya mara 10 katika mwaka huo wa 2016.
Tags
Robert Mugabe
