Msemaji wa ikulu ya White House amesema Rais Donald Trump atatoa
mshahara wake kama hisani kwa mashirika yanayosaidia wasiojiweza katika
jamii.
Sean Spicer amesema anataka waadhishi wa habari wanaoripoti taarifa
kuhusu White House na Rais wa Marekani wamsaidie kuchagua nani wanafaa
kupewa pesa hizo.
Mshahara wa Bw Trump utakuwa umefikia dola 400,000 kufikia mwisho wa mwaka.
Wakati wa kampeni za urais, Bw Trump alisema kwamba hakupanga kupokea
mshahara wake na kwamba badala yake angepokea dola moja pekee ambayo ni
lazima kisheria.
Alikosolewa wakati wa kampeni baada ya taarifa kuibuka kwamba alikuwa
ametoa kiwango kidogo sana cha pesa kama hisani licha ya utajiri wake
mkubwa.
Kuna viongozi wengine walioukataa mshahara?
Bw Trump si kiongozi wa kwanza wa Marekani kukataa mshahara.
Herbert Hoover, aliyekuwa ametajirika kupitia biashara ya madini kabla
ya kuingia madarakani, na John F Kennedy, aliyerithi utajiri mwingi,
wote walikataa kupokea mashahara na badala yake wakatoa pesa hizo
zisaidie wasiojiweza katika jamii.
Meya wa zamani Michael Bloomberg, gavana wa zamani wa California Arnold
Schwarzenegger na gavana wa zamani wa Massachusetts Mitt Romney pia
walikataa kupokea mishahara yao.
Mark Zuckerberg, mwanzilishi wa mtandao wa kijamii wa Facebook, ndiye
mfanyakazi anayelipwa mshahara wa chini zaidi katika kampuni hiyo.
Aidha, ni miongoni wa CEO (Afisa Mkuu Mtendaji) wengi ambao hulipwa mshahara wa $1 pekee.
Sergey Brin na Larry Page wa Google pia wamekuwa wakilipwa $1 kwa mwongo mmoja sasa.
Larry Ellison wa Oracle pia aliukataa mshahara wake kwa miaka kadha
alipokuwa CEO. Afisa mkuu mtendaji wa Hewlett Packard Enterprise (HP)
Meg Whitman apia alichukua hatua sawa.
Viongozi hawa hata hivyo hujipatia pesa kupitia njia nyingine. Wengi ni
kupitia hisa wanazomiliki na wengine hulipwa kwa kutegemea matokeo au
mapato ya kampuni.
Viongozi wa nchi nyingine hulipwa pesa ngapi?
Licha ya $400,000, anazolipwa rais wa Marekani, pia hupewa jumla ya $50,000 ambazo huwa hazitozwi ushuru, kwa mujibu wa sheria.
Waziri mkuu wa Canada alilipwa C$340,800 (£201,202) mwaka uliopita.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alilipwa $242,000 (£193,976) naye
Rais wa Ufaransa Francois Hollande akalipwa $198,700 (£158,000), kwa
mujbiu wa taarifa ya CNN ya mwezi Agosti.
Bw Hollande alipunguza mashahara wake kwa 30% alipoingia madarakani mwaka 2012.
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May hulipwa $186,119 (£143,462) kila
mwaka, ingawa thamani yake kwa dola imeshuka baada ya Uingereza kupiga
kura kujiondoa EU.
Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza David Cameron alishutumiwa sana alipoongeza mshahara wake kwa 10% mwaka 2015.
Hata hivyo alisema jambo la busara ni kulipwa "mshahara unaolingana na kazi".
Aliongeza kwamba kuongezewa mashahara kulimpa uwezo zaidi wa kutoa pesa za hisani na mambo mengine ya kusaidia jamii.
Wazo hili lilitoka wapi?
Mwanzilishi wa Apple Steve Jobs alivumisha wazo la mshahara wa $1 Silicon Valley baada yake kurejea katika kampuni hiyo 1997.
Wakuu wa kampuni mbalimbali wamekuwa wakikosa kupokea mishahara yao tangu Vita Vikuu vya Kwanza na vya Pili vya Dunia.
Wakuu wa kampuni, benki na viwanda mbali ambao walijitolea kutumikia
nchi katika majukumu mbalimbali wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya
Dunia walifahamika kama "wanaume wa dola moja kila mwaka". Kwa kuwa
sheria nchini Marekani huharamisha mtu kufanya kazi bila kulipwa,
viongozi hao walipokea mshahara wa $1 kutimiza matakwa ya sheria kwamba
walikuwa wanalipwa.
Wazo hilo lilirejea wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ambapo wakuu
wa kampuni kubwa kama vile Lockheed, Chrysler na Boeing walijitokeza
kutumikia nchi kama uzalendo.
Tags
TRUMP
