Na Alex Mathias
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Klabu ya Simba, Mwina Kaduguda
amewataka mashabiki wa klabu ya simba na Yanga kuwa makini na mabadiliko
ya mifumo ya uendeshaji shughuli za soka wanayotaka kuyafanya ili
kuhakikisha wanaendelea kupata burudani safi ya soka. Akizungumza na mwaandishi wa habari hii, Jijini Dar es salaam jana, Kaduguda alisema mfumo wa hisa ni mzuri kwa maendeleo ya soka lakini umekuwa ukishusha hali ya ushindani katika timu mbalimbali.
Alisema mashabiki wa Simba hawapaswi kukurupuka katika kufanya maamuzi ya kubadili mfumo huo kwani ipo mifumo mingi yenye uwezo wa kuongeza chachu ya maendeleo ya soka.
Alisema wanachokitaka wanasimba kwa sasa ni furaha kwa kubeba makombe mbalimbali ya mashindano wanayoyashiriki na sio mabadiliko ambayo yanalenga kufaidisha baadhi ya watu.
Kaduguda aliongeza kuwa mfumo unaotaka kufanywa na viongozi wa klabu hiyo kwa sasa utakuwa unatoa nguvu kwa baadhi ya watu kuamua hatima ya mambo ya klabu tofauti na hivi sasa ambapo wanachama ndio wenye jukumu la kutoa maamuzi ya masuala yahusuyo maendeleo ya klabu yao.
Alidai wanachama wa klabu hiyo wanapaswa kuiga mfano kutoka kwa klabu kubwa duniani za Man Chester United pamoja na Arsenal ambazo tangu zilipobadili mfumo wao wameshindwa kuonesha ushindani kama ule uliokuwa ukioneshwa hapo awali.
Alieleza kuwa wadau wengi wanaokuwa na hisa nyingi wamekuwa wakijali
biashara na kukuza vipato vyao badala ya kufikilia namna ya kutwaa ubingwa.
“Huu mfumo sio mgeni kwenye familia ya soka na waathirika wakubwa wa mfumo huu ni Arsenal ambao takribani miaka 13 wameshindwa kuchukua ubingwa,na wakisema wamtimue kocha Arsene Wenger, mwenye hisa nyingi anasema anamtaka huyohuyo kwa sababu anamtengenezea faida kubwa,”alisema Kaduguda.
Pia Kaduguda alisema ni vyema viongozi wa klabu hiyo wakatafuta mfumo mwingine ambao utaleta faida kwa mwenyehisa nyingi, mashabiki pamoja na wanachama wa timu hiyo na siyo ule uliopendekezwa wa kumpa mtu hisa asilimia 49 peke yake.
Tags
MICHEZO