Na. M. M. Mwanakijiji
Kwa baadhi yetu tuliokataa kuvingirisha mikono yetu kuunga mkono
mabadiliko yaliyobinafsishwa kwa mtu mmoja tulijikuta hatuna budi
kumuunga mkono Magufuli tukiamini anawakilisha mabadiliko ya kweli.
Binafsi niliamini kabisa kuwa Taifa lilikuwa linamhitaji kiongozi kama
Magufuli kuweza kulinasua mahali lilipo kuliko kiongozi yule mwingine
toka upinzani. Niliamini kabisa kuwa Magufuli akishika madaraka atakuwa
na kazi kubwa ya kulirejesha Taifa katika misingi yake ambayo inaonekana
ilikuwa imepotea.
Hatua zake mbalimbali za mwanzo kushughulika na kubana matumizi,
kupambana na ufisadi na kuondoa watendaji mizigo a.k.a majipu
kulinifanya niamini kabisa kuwa Magufuli kazi aliyonayo akiendelea na
kasi hiyo basi ndani ya miezi sita tu atakuwa ameleta heshima katika
utumishi wa umma, kurejesha heshima kwa Watanzania na fahari ya taifa
letu kurudishwa. Niliamini kabisa kuwa Magufuli atafanya kazi hii bila
woga, huruma, husuda, wivu, au kusita sita. Kwamba, hatomwangalia
yeyote, popote na kwa lolote. Ndani ya miezi sita hivi na kabla ya ujio
wa bajeti ya kwanza ya serikali yake basi Magufuli atakuwa ameshaweka
alama za namna gani taifa linataka kwenda na kila kiongozi atakuwa
amepata ujumbe.
Nilifanya makosa.
Nilifanya makosa kwa sababu nilidhani hii ni kazi rahisi kwa Rais.
Nilidhani ni kazi ya kutimua huyu, kuondoa yule na kumleta yule
mwingine. Nilidhani ni kazi ambayo akimaliza teuzi mbalimbali basi
atakuwa ameipanga serikali yake kwa ajili ya kuchapa kazi.
Sasa najua kuwa uamuzi wake wa kushughulika na watu kwanza kabla ya
mfumo ni jambo muhimu sana. Ulikuwa ni uamuzi sahihi na unajitahi
kutetewa. Watu ndio hutengeneza mfumo; ni watu ndio ambao hukaa chini na
kufanya maamuzi mbalimbali yenye kuathiri (kwa uzuri au ubaya) uwepo na
utendaji wa mfumo wa utawala. Ukiwa na watu wabovu, wabinafsi na wenye
mwelekeo wa ufisadi basi mfumo utakuwa mbovu, wa kibinafsi na wenye
uelekeo wa kifisadi kwa sababu moja kubwa; wale wenye kuiwamba ngoma
ngozi huivutia kwao! Mfumo wetu wa utawala wa kifisadi ulitengenezwa na
watawala wenye mwelekeo wa kifisadi. Matobo (siyo matundu) kwenye sheria
zetu vilitengenezwa na watu ambao walijua wakiziba na wao watakuwa
wamejizibia.
Magufuli asingeweza kutengeneza mfumo mwingine kwa kutumia watu wale
wale walioutengeneza mfumo huu wa sasa na hasa kama watu hao ni
wanufaika wa mfumo huu. Ingelikuwa ni sawa sawa na kumtaka Rais
awalazimishe watu wakate matawi ambayo wamekalia huku wakijua kwa
kufanya hivyo wataangukia mtoni kwenye mamba wengi. Hakukuwa na jinsi
nab ado hakuna jinsi ni lazima kuwaondoa hawa na kuwashughulikia ili
kuleta watu wenye fikra zinazoakisi mwelekeo wa serikali yake.
Ni kwa sababu hiyo, kumbe kazi ile ya miezi sita kwa kweli haiwezekani.
Ni kazi ambayo inapaswa kuwa endelevu na yenye matokeo bora. Tayari
tumeanza kuona dalili za yaliyomo ndani ya ripot ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu (CAG) na tayari inatisha kama ilivyotisha mwaka 2006 na miaka
iliyofuatia.
Kwa muda mrefu tumekuwa tukijulishwa juu ya uchafu wa watendaji wetu na
taasisi zetu na mara karibu hizo zote tumekuwa tukionesha kushtushwa na
kusikitishwa tukiamini kuwa labda mwaka unaofuatia mambo yatakua
tofauti. CAG aliyepita alikuwa anarudia baadhi ya hoja mwaka baada ya
mwaka na wakati mwingine kuhusiana na taasisi au watu wale wale. Na
safari hii tusije kushangaa kuwa hata CAG wa sasa anaweza kujikuta
amegusa maeneo yale yale; matumizi mabaya ya sheria ya manunuzi ya umma,
fedha kutumiwa bila maelezo, kutopatikana kwa vitabu vya masuala ya
fedha wakati wa ukaguzi, na upotevu wa fedha za umma kwa namna ambayo
inadokeza tu kuwa zimeliwa.
Magufuli basi ana kazi kubwa; kushughulikia viongozi wabadhirifu,
wazembe, wezi, na wenye kutumia madaraka yao vibaya na wakati huo huo
kupanga na kusimamia serikali yake huku akiuunda upya mfumo uliojaribiwa
na kuharibiwa.
Kwa mwendo alioanza nao hakuna shaka yoyote jambo moja lilikuwa sahihi
kwa upande wangu; kuunga mkono mabadiliko haya. Wapo wanadhani hali ni
ngumu sasa na kuwa serikali inabana naamini bado hatujaona hasa ugumu
kwani hadi hivi sasa bado serikali inahangaika na madudu ya nyuma na
yanatisha. Kusahihisha uchumi (correcting an economy) ambao umejengwa na
kusimamiwa na utamaduni wa kifisadi (corrupt culture) haiwezekani kuwa
ni jambo moja.
Ni kwa sababu hiyo naamini:
1. Kuanza kazi kwa mahakama za kushughulikia ufisadi na uhujumu uchumi kunahitajika mara moja
2. Sheria ya CAG ifanyiwe mabadiliko mapema zaidi ili CAG awe na
madaraka ya kutoa agizo la kusimamishwa kazi na hata kufikishwa
mahakamani kwa mtendaji yeyote wa umma ambaye uchunguzi wake (CAG)
unaonesha kuwa kuna uvunjaji wa sheria. Ikiwezekana ofisi ya CAG iwe na
Waendesha mashtaka wake kama ilivyo kwa TAKUKURU. Haipaswi madudu yam
waka mzima yanasubiri mwaka mwingine kujulikana. CAG anapofanya ukaguzi
na kukuta madudu na ushahidi wa kisayansi upo (forensic evidence) basi
hatua zichukuliwe mara moja. Siyo awe na uwezo wa kupeleka mashtaka
lakini kwa kupendekeza kwa DPP au hata yeye mwenyewe washutumiwa watiwe
mbaroni, mali zao zinazohusiwa kupatikana kwa njia haramu kukamatwa ili
zije kufilisiwa wakikutwa na hatia.
3. Sheria ya Usalama wa Taifa inahitaji kufanyiwa marekebisho ya haraka –
hili ni jambo ambalo limekuwa katika mada zangu kwa karibu miaka kumi
sasa. TISS bado ni dhaifu sana na udhaifu wake umechangia sana
kutamalaki kwa utamaduni wa kifisadi. Natumaini Magufuli hatochukua muda
mrefu kuifumua hii taasisi kwani ndio moyo wa taifa. Ikilegea taifa
liko mashakani.
Kuna na mengine mengi ambayo naamini Magufuli atayafanya kwani tayari
ameshaanza kuyafanya na kuwa endapo atafanikiwa tutakapofika mwisho wa
mwaka huu kama taifa tutashusha pumzi kidogo kwani angalau tutakuwa
katika mazingira ya kusema “kweli hakika huyu alikuwa anahitajika”.
Ni wazi pia kutokana na kazi hii ngumu ambayo tunaamini Magufuli
anaiweza kutakuwepo na wasema “hapana” na waleta “vikwazo”. Wale ambao
wataona maslahi yao yanaguswa na kuwa pale walipokuwa wakihemea sasa
panaanza kuondolewa. Watakuwepo watu ambao watajaribu kudhulumu na
kuharibu jitihada hizi; raia wa kawaida, watendaji serikalini, wabunge
na tusije kushangaa hata watu wake wa karibu. La maana ni kukaza mwenzo
na kuendelea kusafisha serikali, kuleta uwajibikani, na nidhamu ili
hatimaye Ujenzi Mpya (Reconstruction) wa taifa letu uanze tena kwani
pale tulipoacha kulijenga tulianza kulibomoa. Hizi ni Zama Mpya, zama za
ujenzi mpya wa taifa letu.
Katika hili, naamini nilikuwa sahihi na bado naendelea kuwa sahihi. Magufuli ni kiongozi wa zama hizi.
Tags
RAIS MAGUFULI
