NYOTA saba wa Simba waliokuwa kwenye timu zao za taifa, wametua kininja
mjini Bukoba kuungana na wenzao kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania
Bara dhidi ya Kagera Sugar, Jumapili hii.
Wachezaji hao ni mshambuliaji, Laudit Mavugo, aliyekuwa na kikosi cha
timu yake ya Taifa ya Burundi, huku wengine Ibrahimu Ajib, Shiza
Kichuya, Jonas Mkude, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Said
Ndemla na Muzamiri Yassini, nao wameungana na wenzao baada ya
kuiwakilisha Taifa Stars kwenye mechi mbili za kirafiki.
Nyota hao baada ya mechi ya juzi ya kirafiki kati ya Tanzania na Burundi
ambapo Stars ilishinda mabao 2-1, jana alfajiri waliondoka jijini Dar
es Salaam na kutua mjini Bukoba asubuhi na mapema wakitumia ndege ya
Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na mara baada ya kutua waliungana na
wenzao kambini bila hata kupumzika na kwenda moja kwa moja mazoezini
kwenye Uwanja wa Taasisi ya Kanisa Katoliki mjini humo.
BINGWA limenasa taarifa za ndani kwamba wachezaji hao waliwekwa
mafichoni na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, baada
ya kumaliza mechi dhidi ya Burundi kukwepa hujuma kabla ya kuondoka nao.
Kutua kwa wachezaji hao Bukoba kumeleta hamasa kubwa kwa nyota wengine
ambao walikwishatangulia na kocha wao Joseph Omog, hivyo waliendelea na
maandalizi ya mchezo huo utakaochezwa siku hiyo ya Jumapili kwenye
Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
“Wachezaji wetu wameingia leo asubuhi kama maninja wakiwa na Kaburu,
walipofika tu kitu cha kwanza cha kufanya walibadili nguo na kuungana na
wenzao mazoezini,” kilisema chanzo kimoja cha habari cha ndani.
“Ujio wao uliamsha hamasa sana, kwani baada ya kuonekana wenzao
waliwafurahia na kuwashangilia na kukumbatiana wakipongezana kwa kile
ambacho kila mmoja ameonyesha kwenye mechi hizo za kirafiki,” kiliongeza
chanzo hicho.
Meneja wa timu hiyo, Mussa Hassan ‘Mgosi’, ameliambia BINGWA jana kuwa
kurejea kwa wachezaji wote saba salama kumeongeza chachu ya ushindani
baina yao kuelekea mechi zao za Kanda ya Ziwa wakianza na Kagera Sugar.
“Wachezaji hao wamefika leo asubuhi (jana) na walipata nafasi ya kufanya
mazoezi pamoja na wenzao ambao walitangulia kufika hapa, kurejea kwao
kumeongeza mzuka na hatuna shaka ya pointi tatu zitapatikana Jumapili,”
alisema.
Vinara hao wa Ligi Kuu, Simba itakuwa Kanda ya Ziwa kucheza mechi tatu
mfululizo, ambapo Jumapili wataanza na Kagera Sugar mjini Bukoba, kabla
ya kwenda Mwanza kukipiga na Mbao FC, kabla ya kuhitimisha ziara hiyo
dhidi ya Toto Africans.
Simba inaongoza msimamo wa ligi wakiwa na pointi 55, huku mahasimu wao,
Yanga wakishika nafasi ya pili kwa kuzidiwa pointi mbili, wakati Azam ni
watatu wakiwa na pointi 44, kila mmoja akiwa amecheza mechi 24.
Credit - Bingwa
