Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Serikali inaendelea na operesheni
ya kukagua viwanda vinavyotengeneza pombe zilizo kwenye vifungashio vya
mifuko ya plastiki maarufu kama “viroba” ili kujiridhisha kama viwanda
hivyo vimesitisha uzalishaji wa pombe hizo pamoja na kuzuia utokaji wa
pombe ambazo bado zipo katika maghala.
Hayo yamesemwa na Mwanasheria wa
Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Manchale Heche
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari wakati wa operesheni hiyo
ambayo inaendelea Jijini Dar es Salaam.
“Zoezi linaendelea kama
lilivyoanza jana ambapo tunakagua viwanda vinavyozalisha viroba, na
mpaka sasa tumeshatembelea viwanda vitatu ambavyo ni kiwanda cha Kibo
Spirit kinachotengeneza pombe ya kiroba aina ya Double Panch, Kiwanda
che Blue Nile kinachotengeneza viroba vya Kitoko na Rivella pamoja na
kiwanda cha True Bell kinachotengeneza viroba vya Bonanza na Suke,”
alifafanua Heche.
Aliendelea kwa kusema kuwa lengo
la operesheni ni kukagua viwanda vyote vinavyozalisha pombe aina ya
viroba ili kujiridhisha ikiwa viwanda hivyo vimetekeleza agizo la
Serikali la kusimamisha uzalishaji wa pombe hizo kuanzia Machi 01, mwaka
huu.
Heche amesema kuwa operesheni
hiyo pia inahusisha ukaguzi kutambua idadi ya pombe zilizobaki katika
maghala mbalimbali na kuzuia pombe hizo kutotolewa katika maghala hayo
mpaka hapo Serikali itakapotoa agizo ya namna ya kuziharibu pombe hizo.
Aidha amesema kuwa agizo limetoka
katika mipaka yote ya nchi kuzuia uingizaji wa pombe hizo na
kuzirudisha nchi zilizotoka kwa gharama za muhusika aliyesafirisha pombe
hizo.
Kwa upande wake Meneja Uendeshaji
wa Kiwanda cha True Bell (T) Limited kilichopo Shekilango, Godwin
Mungere amesema kuwa kiwanda hicho bado kilikuwa katika majaribio lakini
kutokana na agizo la Serikali wamesitisha uzalishaji wa pombe za viroba
ambapo wao walikuwa wakizalisha viroba aina ya Bonanza na Suke.
Ameeleza kuwa akiba ya pombe za
viroba vilivyobaki katika ghala lao ni katoni 166 za viroba vya Bonanza
na katoni 165 za viroba vya Suke ambapo wanasubiri maelekezo kutoka
Serikalini namna ya kuharibu pombe hizo.
Nae, Mkurugenzi wa Kibo Spirit
kilichopo Sinza kwa Remmy Muhid Mwacha amesema kuwa kiwanda hicho
kilikuwa bado kipo kwenye majaribio ya kutengeneza viroba aina ya Double
Panch lakini kwa sasa hawaendelei na uzalishaji wa pombe hizo ila
kiwanda hicho kwa sasa kinazalisha maji ya kunywa ya Kibo Cool.
Operesheni ya viroba ilianza
rasmi jana kwa mkoa mzima wa Dar es Salaam ambapo ni utekelezaji wa
agizo la Serikali la kuzuia uzalishaji, usambazaji na utumiaji wa pombe
hizo kuanzia Machi 1, mwaka huu. Adhabu ya kutumia, kusambaza au
kuzalisha pombe hizo ni faini inayoanzia shilingi elfu 50 mpaka milioni 5
na kifungo cha kuanzia miezi 3 mpaka miaka 3 jela.
Tags
POMBE ZA VIROBA