Hatua ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutoa siku 14 kwa Shirika
la Umeme Zanzibar (Zeco) na taasisi za Serikali kuhakikisha wanalipa
madeni yao ya umeme la sivyo watakatiwa umeme, vitaipa wakati mgumu
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka aliwaambia
waandishi wa habari kwamba shirika lake linadai wateja hao jumla ya
Sh275 bilioni.
“Tunadai kiasi kikubwa sana cha fedha kutoka kwa wateja wakubwa na
wadogowadogo, mpaka Zeco, hivyo tunatoa notisi ya siku 14 kuanzia leo
(jana) walipe deni lao kwani baada ya hapo tutasitisha huduma pamoja na
kuchukua hatua nyingine za kisheria,” alisema Dk Mwinuka.
Katika kiasi hicho, Zeco inadaiwa Sh127 bilioni ambacho ni sawa na
asilimia 15 ya Bajeti ya Serikali ya Zanzibar kwa mwaka 2016/17 ambayo
ni Sh841.5 bilioni.
Pia kiasi hicho ni kikubwa karibu mara nne ya kile kilichotengwa katika
bajeti hiyo kwa ajili ya mikopo ya ndani ambacho ni Sh33.0 bilioni hali
inayoonyesha kwamba Zeco na SMZ watalazimika kuandaa mpango mkakati wa
kulipa deni hilo ambao utamaanisha kujifunga mkanda ili kulimaliza.
Alipoulizwa kuhusu notisi hiyo ya kulipa deni, Waziri wa Ardhi, Maji,
Nishati na Mazingira wa Zanzibar, Salama Aboud Talib ambaye alikuwa
ziarani Pemba alisema hadi jana hakuwa amepokea barua kutoka Tanesco
hivyo asingeweza kuzungumza chochote.
Wiki iliyopita, akiweka jiwe la msingi katika kituo cha kupoza umeme cha
njia ya Kv 132 mkoani Mtwara, Rais John Magufuli aliiagiza Tanesco
kuwakatia umeme wadaiwa wote sugu ikiwamo Zanzibar. Alisema shirikia
hilo halipo kisiasa, hivyo wadaiwa wote wakatiwe umeme.
Sambamba na hayo, alilitaka shirika hilo kutoingia mikataba na kampuni
zinazoweza kusababisha au kuongeza madeni, badala yake mwekezaji yeyote
akitaka kuwekeza azalishe umeme wake na kuuza mwenyewe.
Wadaiwa wengine
Kuhusu wadaiwa wengine, Dk Mwinuka alisema hadi kufikia Januari, shirika
hilo lilikuwa linazidai wizara na taasisi za Serikali kiasi cha Sh52
bilioni huku kampuni binafsi na wateja wadogo wakidaiwa jumla ya Sh94
bilioni.
Alisema malimbikizo hayo ya madeni yamekuwa yakikwamisha jitihada za
utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya msingi ndani ya shirika kwa wakati
ikiwamo uendeshaji, matengenezo ya miundombinu pamoja na miradi
mbalimbali.
Alisema kulipwa kwa malimbikizo hayo ya madeni kutaisaidia Tanesco
kujiendesha kiushindani na kwa ufanisi zaidi, hivyo kuendelea kuchochea
kasi ya ukuaji sekta mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme nchini.
Alipoulizwa kuhusu mashirika na taasisi za umma zinazodaiwa malimbikizo
hayo ambayo Tanesco haikuyataja, Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas
alisema mashirika hayo yanatakiwa kuanza kutekeleza agizo hilo kwa
kulipa deni kama wanavyodaiwa.
Tags
ZANZABAR
