WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimechukua maamuzi magumu katika
historia ya chama hicho tangu kizaliwe kwa kuwafukuza viongozi wa juu
wengi kwa wakati mmoja baada ya kubainika kukiuka misingi ya Katiba ya
chama hicho, gazeti hili limebaini sababu zaidi za kufukuzwa kwa
viongozi hao.
CCM juzi ilitangaza uamuzi mzito wa kuwafukuza uanachama, kuwavua
uongozi na kuwapa onyo kali vigogo 22 ambao wamechangia kukihujumu na
kukifanya chama hicho kinuke mbele ya jamii.
Kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), CCM imeamua kuchukua hatua hiyo
ya kuadhibu viongozi wake baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Kamati Kuu
(CC) iliyokutana jana asubuhi ambayo nayo ilipokea ripoti kutoka kwenye
Kamati Ndogo ya Maadili naNidhamu ya chama iliyoketi mjini hapa juzi.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamprey Polepope ndiye
aliyeutangazia umma uamuzi huo na kusema adhabu hizo zimeanza jana. Muda
mfupi baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo, chanzo cha kuaminika kutoka
Dodoma (jina kapuni) kililidokeza gazeti hili kuwa hatua hiyo imetokana
na usaliti mkubwa uliofanywa na viongozi hao wakati wa uchaguzi mkuu wa
Oktoba 2015.
Chanzo hicho kilisema kutokana na usaliti huo, CCM ilijikuta ikipata
wakati mgumu wa kukubalika katika baadhi ya maeneo kutokana na kuonekana
kinanuka na kutokubalika kwa wananchi wa maeneo hayo.
Hatua hiyo mbali ya kumpunguzia kura aliyekuwa mgombea urais wake Rais
John Magufuli, pia ilikifanya chama hicho kupoteza nafasi nyingine
mbalimbali ikiwemo ubunge na udiwani.
Usahihi wa taarifa hizo ulithibitishwa wakati wa mkutano wa Polepole na
waandishi wa habari ambapo Katibu huyo wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM
alisema; “Ukiona mwanachama amefukuzwa ndani ya chama maana yake
amefanya kosa kubwa.
“Mtu huyo atakuwa amefanya kitendo cha usaliti kilichosababisha chama
kunuka au chama kushindwa na wanaCCM kumuona si mwenzetu na hakubaliki
tena.” Waliofukuzwa uanachama Polepole aliwataja wenyeviti wa mikoa
waliofukuzwa uanachama kuwa ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa Jesca
Msambatavangu, Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida,
Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga, Erasto Kwilasa na Mwenyekiti wa Mkoa wa
Mara, Christopher Sanya.
Alisema katika kundi hilo la waliofukuzwa pia wamo Wajumbe wa NEC (Mnec)
wa Wilaya ya Babati Ally Khera Sumaye na Wilaya ya Arumeru Mathias
Manga. Wengine ni wenyeviti wa wilaya, ambapo lungu hilo limetua kwa
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Arusha Wilfred Ole Soilel Molel,
Mwenyekiti wa Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge, Mwenyekiti wa Wilaya
ya Longido Makolo Laizer, Mwenyekiti wa Wilaya ya Babati Ally Msuya na
Mwenyekiti wa Wilaya ya Gairo Omar Awadh.
Wengine waliokumbwa na adhabu hiyo kubwa na ya juu kabisa kwa CCM ni
Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake (UWT) Taifa na Mbunge wa Viti Maalum,
Sophia Simba. Kutokana na tukio hilo Simba pia amepoteza sifa ya kuwa
Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia jumuiya hiyo.
Hata hivyo siku chache zilizopita mwana CCM huyo alitangaza nia yake ya
kutogombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa
kuanza hivi karibuni na kumalizika ifikapo Desemba mwaka huu.
Hata hivyo katika historia CCM imewahi kuwafukuza uanachama viongozi wa
juu zaidi katika uongozi kama ilivyowahi kufanywa mwaka 1988, pale
ilipomfukuza Maalim Seif Shariff Hamad akiwa Waziri Mkuu Kiongozi wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.Miaka 10 baadaye yaani mwaka 1998
ilimfukuza uanachama Hamad Rashid Mohammed.
Waliovuliwa nafasi za uongozi, kuonywa Adhabu hiyo ya NEC ya CCM
haikushia hapo kwani chama hicho kilitangaza kuwavua nafasi za uongozi
baadhi ya viongozi wake kwa makosa hayo ya kukiuka misingi ya Katiba ya
chama hicho.
Wajumbe waliovuliwa uongozi ni Mnec kutoka Wilaya ya Tunduru Ajili
Kalolo, Mnec wa Wilaya ya Singida Mjini Hassan Mazala na Mnec wa Wilaya
ya Kibaha Mjini Valerian Burreta.
Aidha chama hicho kimetoa onyo kali kwa viongozi wengine ambapo
waliokumbana na onyo hilo na ambao watakuwa kwenye uangalizi kwa muda wa
miezi 30 ni pamoja na Mnec kutoka Wilaya ya Kilwa, Ali Mchumo.
Wengine ni Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kigoma na Mbunge wa Viti Maalum,
Josephine Gezabuke, Mwenyekiti wa Wilaya ya Muleba Muhaji Bushakonyo,
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Iringa Mjini Abeid Kiponza na wa Wilaya
ya Singida Mjini Hamisi Nguli.
Aidha katika kuonesha kuwa haikufanya mzaha katika kufikia uamuzi huo,
CCM pia imetoa adhabu kwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Balozi Emmanuel Nchimbi
ambaye amepewa onyo kali na kutakiwa kuomba radhi mara moja, huku mjumbe
mwingine wa Kamati Kuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma
na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Adam Kimbisa akisamehewa.
Nini hatma yao Polepole akizungumzia hatma ya waliopewa adhabu hiyo
alisema pamoja na kwamba wamezuiwa kukata rufaa kupinga uamuzi huo wa
NEC, lakini bado wanayo fursa ya kuwa wanaCCM au kuwa tena viongozi
baada ya kujirekebisha kwa kipindi fulani, kwa mujibu wa Katiba ya chama
hicho.
Alisema kwa waliovuliwa madaraka au kupewa onyo watakuwa katika kipindi
cha uangalizi kisichopungua muda wa miezi 30 ili kuona kama wataweza
kujirekebisha huku akisema kwa waliofukuzwa wanaruhusiwa kuomba tena
uanachama wa CCM baada ya kupita miaka minne au miezi 48.
“Kwa hali hiyo hawa walioonywa au kuvuliwa madaraka wanakosa haki ya
kushiriki katika uchaguzi wa ndani ya chama utakaofanyika kuanzia
mwishoni mwa Machi hadi mwanzoni mwa Desemba mwaka huu na uchaguzi
mwingine katika kipindi cha adhabu,” alisema Polepole.
Zanzibar yaundiwa Kamati Akizungumzia hali ilivyo kwa upande wa
Zanzibar, Polepole alisema Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula
ataongoza kamati kwenda Zanzabar kuchunguza mwenendo wa chama, uchaguzi
na maadili ya wanachama.
Alisema kamati hiyo itakuwa na wajumbe Pandu Amri Kificho, Shamsi Vuai
Nahodha, Maua Daftari, Daud Issa, Suleiman Saharani, Steven Wasira,
Hadija na Zakhia Meghji. Alisema kamati hiyo itafanya kazi ya kuchunguza
hali ya kisiasa, uchaguzi ulivyofanyika Zanzibar na maadili ya
wanachama katika kisiwa hiyo, na kwamba taarifa yake itatolewa baadaye.
Ushiriki Mkutano Mkuu Polepole alisema viongozi ambao chama kimewafukuza
uanachama, hawataruhusiwa kuingia kwenye mkutano mkuu wa leo, isipokuwa
chama kitawapa malazi, chakula na eneo la kulala na kutakiwa kurudi
makwao.
“Kwa vile CCM ni chama kinachotambua utu na kuzingatia haki, wajumbe
hawa watapatiwa sehemu ya kulala, chakula na haki zao nyingine na kesho
(leo) watatakiwa kurudi makwao. “
Tayari viongozi hao ambao walikuwa wakimiliki mali za chama, wahusika
wameshawatembelea na kuwajulisha kwamba wanatakiwa kuziacha na
kuondoka,” alisema. Polepole alisisitiza kuwa CCM imechukua uamuzi huo
wa kihistoria wa kuwaadhibu viongozi wake, kama sehemu ya mkakati wake
wa kufanya mabadiliko na kuwa chama cha wanachama zaidi.
Magufuli asisitiza mabadiliko Awali akifungua mkutano wa NEC, Mwenyekiti
wa CCM Taifa, Rais Magufuli aliwataka wajumbe wa NEC kukubali
mabadiliko yanayofanywa na chama hicho yakiwamo ya kupunguza wajumbe
wake 200 kati ya 358 na kubaki wajumbe 158.
Rais Magufuli alisisitiza kwamba wanachama wanatakiwa kukubali mageuzi
yanayofanyika ndani ya chama hicho ili kukiletea chama hicho mageuzi ya
kweli. “Katika mageuzi haya kuna viongozi na wajumbe wa mkutano
watapunguzwa wakiwamo makatibu wa CCM katika ngazi mbalimbali zikiwamo
za wilaya na mikoa ambao si lazima wawe wajumbe wa mkutano wa NEC.
“Watu wanasema lazima Makatibu wa CCM Mkoa wawe wajumbe wa mkutano wa
NEC, mimi nasema si lazima kama wanataka kuwa wajumbe waende wakagombee
uenyekiti,” alisema.
Huku akishangiliwa na baadhi ya wajumbe, Magufuli alisema, kama suala la
uwakilishi wa makatibu si lazima, kutokana na ukweli kwamba mwaka jana,
wakati Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete akiingia ukumbini waliimba
kwamba wana imani na mtu mwingine badala ya Mwenyekiti anayewalipa
mshahara.
Mwenyekiti akauliza, kwanini makatibu ambao ni waajiriwa hawakusimama na
kupigana au kupinga kitendo cha kuimba kwamba watu wana imani na mtu
mwingine wala si Mwenyekiti wao wakati ndiye anayewalipa mshahara.
Magufuli alisisitiza kwamba kama makatibu wanataka kuwa wajumbe,
wasuburi wakagombee katika nafasi mbalimbali zikiwamo za uenyekiti,
lakini kwa sasa si lazima kuwa wajumbe.
Tags
CCM
