KATIKA historia yake ya miaka 50 na ushee, Tanzania haijawahi kuwa na
Mke wa Rais, mstaafu au aliye madarakani, bungeni. Wiki iliyopita, Rais
John Magufuli akaweka historia mpya kwa kumtangaza Salma Kikwete, mke wa
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, kuwa Mbunge wa Kuteuliwa.
Na Mama Salma si First Lady wa kawaida. Kwenye historia ya miaka 50
hiyohiyo, Tanzania haijawahi kuwa na mke wa Rais ambaye ni mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwaka juzi, nilikuwa ndani ya ukumbi wa Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma
wakati wa kinyang’anyiro cha kutafuta mgombea urais kupitia chama hicho.
Mama Salma alikuwa amekaa pembeni ya Benard Membe aliyekuwa mmoja wa wagombea waliokuwa wakipewa nafasi kubwa kushinda.
Wakati wake wa marais waliopita wa Tanzania walikuwa hawatajwi katika
vinyang’anyiro vya namna hii; haikuwa siri kwamba Salma alikuwa akitaka
Membe ndiye awe Rais wa Tanzania baada ya Kikwete.
Na ndiyo sababu, ilikuwa ikijulikana kuwa Membe huyohuyo ndiye alikuwa
chaguo la Kikwete mwenyewe. Na hii ni kwa sababu, haingewezekana kwa
Salma kupiga kampeni hadharani kwa mtu ambaye mumewe hamuungi mkono.
Mara baada ya Magufuli kumtangaza Salma kuwa mbunge, nilichora kwenye
karatasi duara moja lililozungukwa na miduara mingine mingi. Lengo langu
lilikuwa kutafuta sababu hasa za Rais kufanya uteuzi ambao hakuna
aliyekuwa akiutarajia.
Uteuzi wa Salma unahitaji tafakuri ya kipekee. Huyu ni mwanasiasa ambaye
tayari ameshiriki katika siasa za juu kabisa za taifa letu. Kama ana
ndoto au mpango wowote ule, hauwezi kuwa mpango wa mambo madogo madogo.
Tafakuri yangu ilinifikisha pia katika tukio lilitokea mwishoni mwa wiki
hiyohiyo; wakati Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Sofia
Simba, alipotangaza kuwa hatawania tena nafasi hiyo.
Salma, anaweza kabisa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa UWT. Hii ni kwa sababu
sasa anakijua chama chake vizuri, anajulikana miongoni mwa akinamama
nchini na kwa sababu ya mumewe, tayari ana kada maarufu wa chama nyuma
yake.
Na kama Salma atakuwa Mwenyekiti wa UWT, maana yake ni kwamba atakuja
kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Ukichanganya na nafasi yake bungeni,
maana yake ni kwamba atakuwa na fursa pana ya kukutana na watu na
makundi mbalimbali.
Hadi sasa, mwanamke mwenye madaraka makubwa kuliko wote hapa nchini ni
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. Kwenye siku za karibuni, ushawishi
wake katika jamii umekuwa ukiongezeka kila kukicha.
Kuna wanaoamini kwamba tayari ana sifa za kumrithi Dk. Ali Mohammed
Shein kwenye uchaguzi ujao wa Zanzibar na kuna wanaoamini kwamba kama
Tanzania iko tayari kwa Rais wa kwanza mwanamke, Samia yuko katika
nafasi nzuri sasa kuliko mwanamke mwengine yoyote.
Ujio wa Salma kwenye siasa, unapunguza kidogo nguvu ya ushawishi wa
Samia. Ni wazi kwamba Kikwete alipigiwa kura nyingi na wanawake wakati
akitafuta urais na ni rahisi kwa mapenzi hayo kuhamia kwa Salma.
Pia, miaka tisa ijayo, watoto wa kike ambao walisomeshwa na Salma
kupitia taasisi yake ya Wanawake na Maendeleo (Wama), watakuwa watu
wazima ambao wana ushuhuda wa namna mama huyu alivyowasaidia.
Hata hawa wasanii maarufu wa kike na kiume hapa nchini ambao kwa sasa
wanaonekana kumuunga mkono Samia, watahamia kwa Salma kirahisi tu kama
Kikwete atataka hivyo.
Hii ni kwa sababu, hakuna kiongozi mwengine hapa nchini anayeweza
kujidai kuwa na ushawishi mkubwa kwa wasanii hapa nchini kuliko Jakaya.
Kama Magufuli angeacha hali ya sasa (status quo) iendelee, ni wazi kuwa
Samia ndiyo angekuwa mwanamke mwenye ushawishi mkubwa kuliko mwengine
yeyote hapa nchini kuelekea 2020 na 2025.
Hadi sasa, hakuna anayejua sababu hasa za Magufuli kumteua Salma kuwa
mbunge. Kwa wanaofahamu siasa za CCM zilivyo sasa, si siri pia kwamba
hatua hii inaonekana kuwa na lengo la kukiweka chama pamoja.
Lakini, wakati nachora duara zangu za kuangalia nje ya boksi, nimeona
pia kwamba hatua hii ya Magufuli –hata kama pengine yeye hakuwa na
dhamira hiyo, inapunguza ushawishi wa kisiasa wa Makamu wake wa Rais
walau kwa Tanzania Bara.
Bila shaka, kuanzia siku ambayo Salma ataapishwa rasmi kuwa mbunge,
ramani mpya ya michezo ya kisiasa ndani ya CCM itaanza kuchorwa.
Na kwa kuanzia, wiki ijayo, nitaeleza namna kinyang’anyiro cha kuwania
urais kumrithi Magufuli kitakavyoathiriwa na uteuzi huu wa sasa wa Mama
Salma Kikwete.
Imeandikwa na Ezekieli Kamwaga wa Raia Mwema
Tags
SIASA
