VINASABA vya faru John vinatarajiwa kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa
vipimo vya vinasaba (DNA ) muda wowote kuanzia wiki hii baada kupatikana
kwa mfadhili wa kulipia gharama za vipimo hivyo,
Faru John alizua gumzo nchini mwishoni mwa mwaka jana baada ya Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa, kufanya ziara katika Hifadhi ya Bonde la
Ngorongoro (NCAA) na kuwatuhumu maofisa wa shirika hilo na wale wa Idara
ya Wanyamapori kwa ‘kumuuza’ faru John kwa kampuni ya Grumeti kwa
takriban shilingi milioni 200.
Kutokana na tuhuma hizo maofisa zaidi ya watano kutoka Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro, Idara ya Wanyapori na Tawiri walitiwa mbaroni kwa
mahojiano na vyombo vya usalama. Hata hivyo, baada ya muda maofisa hao
waliachiwa huru.
Kampuni hiyo ya Grumeti ambayo imewekeza katika shughuli za biashara ya
hoteli, utalii na uhifadhi inamiliki hifadhi ndogo (sanctuary) ya Faru
Weusi pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Aidha katika mfululizo wa matukio kuhusu sakata la faru huyo baadaye
ilibainika alifariki dunia Agosti mwaka jana na waziri mkuu aliunda
kamati maalumu kuchunguza kifo chake na pia kupimwa DNA.
Taarifa zilizofika kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii
zimeeleza kuwa tayari nyaraka zote muhimu kuhusu kupelekwa kwa vipimo
hivyo nchini humo zimekamilika.
Habari zaidi zinaeleza kuwa pamoja na kukabidhi nyaraka, maofisa wa
Wizara ya Maliasili na Utalii watakabidhi pia sampuli za vinasaba hivyo
kwa ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili visafirishwe kwenda Afrika
Kusini.
Awali ilidaiwa kuwa kulikuwa na hali ya utata kuhusu nani hasa atalipa
gharama za vipimo hivyo vya DNA baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii
kushindwa kupata fedha za kugharimia vipimo hivyo.
“Taarifa ni kwamba kuna mfadhili amepatikana (hakutaja jina) na kulipia
gharama za vipimo vya DNA nchini Afrika Kusini katika maabara ya kupima
vinasaba ambayo iko kitivo cha wanyama katika Chuo Kikuu cha Pretoria,”
kilieleza chanzo chetu ndani ya Wizara hiyo.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa gharama za vipimo hivyo ni katika ya dola
za Marekani 300,000 hadi 500,000 ambazo ni zinaweza kufikia kati ya
shilingi za Tanzania milioni 700 hadi bilioni moja.
“Kwa kweli gharama za kufanya vipimo vya DNA ziko juu sana na serikali
haikuwa na fedha zilizotengwa kwa kazi hiyo, amepatikana mfadhili ambaye
atalipia gharama hizo hivyo muda wowote kuanzia sasa vipimo vitapelekwa
Afrika Kusini baada ya kukamilika kwa nyaraka zote muhimu,” alieleza
mmoja wa maofisa wa wizara hiyo aliyeomba asitajwe jina gazetini kwa
kuwa si msemaji wa suala hilo.
Majibu ya vipimo hivyo ndiyo yanayotarajiwa kutengua kitendawili cha
iwapo sampuli za vinasaba zilizochukuliwa kutoka katika mabaki ya mnyama
huyo zinaoana na zile zilizoko kwenye pembe yake na kujua iwapo faru
huyo alikufa kama watendaji wa Idara ya Wanyapori wanavyodai au la.
Juhudi za kumpata msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dorina Makaya
hazikuweza kufanikiwa kutokana na simu yake kutokuwa hewani kwa muda
mrefu lakini Afisa Mawasiliano wa Wizara hiyo, Hamza Temba, alisema kwa
kifupi kuwa suala hilo liko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na pia Mkemia
Mkuu wa Serikali.
“Sidhani kama jambo hilo liko chini ya wizara kwa kifupi ninavyofahamu
suala hilo liko chini ya ofisi ya waziri mkuu na pia mkemia mkuu wa
serikali,” alisema ofisa huyo.
Maabara ya Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini ( Veterinary
Genetics Laboratory – VGL)) kwa mujibu wa mtandao wa
researhmatters.up.ac.za ilianzishwa mwaka 2009 baada ya kuwapo kwa wimbi
kubwa la ujangili dhidi ya wanyama hao nchini humo.
Kwa mujibu wa mtandao huo wataalamu wa chuo hicho kitivo cha utafiti na
tiba ya wanyama wakiongozwa na Dk. Cindy Harper walifikia uamuzi wa
kuanzisha maabara hiyo kwa lengo la kukusanya sampuli za vinasaba kutoka
kwa wanyama hao na kuhifadhi katika kanzidata (database) ya maabara ili
zitumike kama sehemu ya ushahidi mahakamani katika kesi za ujangili wa
faru.
Ugunduzi na uamuzi wa wataalamu hao ulitokana na kesi nyingi dhidi ya
majangili kukwama na wengi kuachiwa huru baada ya kukosekana kwa
ushahidi dhidi yao.
Kwa mujibu wa mtandao huo wataalamu hao wa chuo hicho hutumia sampuli za
vinasaba na kuoanisha na alama za vidole vya majangili kisha kuwapa
waendesha mashitaka ili kujenga ushahidi thabiti wa kuwatia hatiani
washitakiwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa dunia ina faru wasiozidi 29,000 kati ya faru
500,000 waliokuwepo mwanzoni mwa karne ya 20 na Afrika Kusini ndiyo nchi
inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama hao kwa sasa.
Kutokana na ujangili wa muda mrefu dhidi ya faru na mahitaji ya pembe
zake katika nchi za kiarabu na zile za Asia ya Kusini ambazo wakati
mwingine hutumika kama dawa za kiasili kumesababisha dunia kubakiza
karibu asilimia moja tu ya faru.
Nchini Afrika Kusini pekee kati ya mwaka 2010-2015 zaidi ya faru 500
waliuawa na majangili na mwaka 2013 ulivunja rekodi kwa faru 1,008
kuuawa na majangili.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe,
alishindwa kulitolea ufafanuzi suala hilo kwa maelezo kuwa alikuwa
katika kikao cha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na
Maliasili.
Tags
AAH
