Wananchi wakitoa maoni kwa
wataalamu kutoka TGDC na TANESCO wakati wa mkutano wa kujadili athari na
faida za mradi wa jotoardhi wa Ngozi kweye mazingira na kwa jamii.
Mtaalamu wa Sosholojia Bi.
Vaileth Kimaro akizungumza na vikundi vya wanawake wakati wa kujibu
maswali na kupokea maoni kuhusu athari na faida za mradi wa jotoardhi wa
Ngozi kwa jamii na mazingira.
Mhandisi Leonard Masanja
(aliyesimama kushoto) akijibu hoja za wananchi wa Kata ya Ndanto wakati
wa mjadala wa athari na faida za mradi wa jotoardhi wa Ngozi kwa jamii
na mazingira, aliyeshika kipaza sauti ni Afisa Maendelea ya Jamii wa
Wilaya ya Rungwe Bi. Rachel Mbelwa
………………….
Na Johary Kachwamba -TGDC
Wananchi wa Wilaya za Rungwe
na Mbeya Vijijini pamoja na wadau wengine wa mradi wa jotoardhi wa Ngozi
wametoa maoni mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuuliza maswali ya msingi
kabla ya zoezi la uchorongaji visima vya uchunguzi na baadae uvunaji
mvuke wa kuzalisha umeme utakaotokana na nishati ya jotoardhi.
Wananchi walipata fursa ya
kutoa maoni yao kati ya tarehe 6 hadi 11 Machi, 2017, wakati timu ya
wataalamu wa Mazingira na Jamii kutoka Kampuni ya kuendeleza Jotoardhi
Tanzania (TGDC) na TANESCO walipotembelea eneo la mradi, ikiwa ni
matakwa ya kisheria ya kushirikisha wadau na jamii itakayopitiwa na
mradi husika, wakati wa kufanya tathmini ya athari za mradi katika
mazingira na jamii.
Maoni yao ilikuwa ni pamoja na
kuiomba Serikali kusimamia taratibu za ajira wakati wa zoezi la
uchorongaji visima vya jotoardhi, akizungumza Ndugu Yohana Julius wa
Kata ya Swaya Vijijini alisema “wanaomba ajira zisizohitaji ujuzi
wapatiwe wakazi wa eneo la mradi ili wanufaike moja kwa moja kwa
kujiongezea kipato”
Bibi Mary Gwamaka alisema
“wanaomba mradi huu usiwaache nyuma wakina mama, kwani wanao uwezo wa
kufanya kazi mbalimbali, hivyo wanaomba wasibaguliwe”
Akijibu moja ya maswali ya
wananchi, Mhandisi wa Mazingira kutoka TANESCO Bw. Fikirini Mtandika
alisema sheria na taratibu zote za mazingira zitazingatiwa wakati wote
wa utekelezaji wa mradi chini ya usimamizi wa Baraza la Udhibiti na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais –
Mazingira.
“TGDC inaandaa mikakati
mbalimbali ya kupunguza na kuziondoa kabisa baadhi ya athari za mradi
huu katika mazingira yetu” aliongezea Mhandisi Mtandika.
Wananchi wa maeneo yote
yanayozunguka mradi wa jotoardhi wa Ngozi wameridhia hatua ya
uchorongaji visima vya uchunguzi na baadae uzalishaji umeme na wako
tayari kutoa ushirikiano. Kata zinazopitiwa na mradi huu ni Ijombe,
Swaya-Mbeya vijijini, Swaya Rungwe na Ndanto.
Tags
NISHATI / MADINI