WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi wazingatie sheria za Taifa
husika na kamwe wasijihusishe na biashara haramu ya dawa za kulevya.
“Vita ya dawa za kulevya ni kubwa,
hata hivyo Serikali tunaendelea kupambana nayo. Nchi ilikuwa inapoteza
vijana ambao walikuwa wamejiingiza katika biashara haramu ya dawa za
kulevya. Nawaomba msithubutu kuingia huko mtafungwa,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumatano, Machi 22, 2017) wakati akizungumza na Umoja wa Watanzania
wanaoishi nchini Mauritius katika mkutano alioutisha kwenye hoteli ya
Meridien mjini Port Louis.
Amesema katika kudhibiti biashara
hiyo haramu ya dawa za kulevya Serikali iliamua kuunda Mamlaka ya Kuzuia
na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na inafanya kazi vizuri. “Na
tutakamata kila mtu anayejihusisha na biashara hiyo bila kujali cheo,
uwezo na mamlaka aliyonayo,”.
Amesema mamlaka hiyo inafanyakazi
ya kutafuta wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara, lengo likiwa ni
kuokoa vijana ambao wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na madhara
waliyoyapata baada ya kutumia dawa za kulevya.
Katika hatua nyinngine, Waziri
Mkuu amewataka Watanzania hao walioko nchini Mauritius kujenga
mshikamano wa pamoja na wawe na uzalendo na nchi yao. Pia wawe mabalozi
wazuri wa kutangaza vivutio vya Taifa.
Amesema ni vema wakatumia fursa
walizonazo katika kutafuta wawekezaji na kuwashawishi waje nchini na
kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, uvuvi, nishati na
utalii.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha
na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed
amewaomba Watanzania hao wazidishe mshikamano miongoni mwao kwa kuwa
umoja wao ndiyo nguzo yao.
“Mko hapa kwa ajili ya kutafuta
elimu na wengine mnafanya kazi, shughuli ambazo zitawasaidia kuboresha
maendeleo yenu na Taifa kwa ujumla, hivyo nawaomba mzingatie
kilichowaleta,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa muda wa Umoja
wa Watanzania waishio nchini Mauritius, Bw. Donald Kongwa ambaye ni
Ofisa wa benki ya Standard Chaetered nchini Mauritius amemuhakikishia
Waziri Mkuu kwamba kipato wanachokipata watakitumia kwa kuwekeza
Tanzania kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa.
Aidha, amesema wanaunga mkono na
kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika
kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, ujenzi
wa miundombinu ya kisasa, ununuzi wa ndege pamoja na kuimarisha
uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wa umma.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MACHI 22, 2017.
Tags
MADAWA YA KULEVYA