Hatimaye Kilio cha Wazanzibara
kimepata jibu baada ya mkutano mkuu wa 39 wa Shirikisho la soka barani
Afrika (CAF) unaoendelea mjini Addis-Ababa, Ethiopia, umepitisha ombi la
chama cha soka Zanzibar (ZFA) kuwa mwanachama rasmi wa CAF.
Ni jambo la kihistoria kwa
Zanzibar kwani safari hii ombi lao limepitishwa bila kupingwa na inakuwa
nchi ya 55 mwanachama wa kujitemea wa CAF.
Awali Zanzibar ilikuwa
inaunganishwa na Tanzania bara chini ya TFF na kupelekea kukosa haki za
kushiriki kama nchi kwenye mashindano yanayoandaliwa na CAF pamoja na
yale ya FIFA.
Pendekezo hilo lilipelekwa na Rais
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndugu, Jamal Malinzi na
lilipokelewa na wajumbe 54 wengine waliokuwepo.
Hii maana yake ni kuwa kwa sasa
CAF ndio shirikisho mwanachama wa FIFA kwa upande wa mabara lenye
wanachama wengi zaidi kuliko wote.
Vilabu vya Zanzibar vimekuwa
vikishiriki mashindano mbalimbali ya CAF lakini kwa ngazi ya kitaifa
hawakuwa na ruhusa na walicheza kwa kuungana na Tanzania bara na
kushiriki kama Tanzania.
Kwa maana hiyo basi, chama cha
soka cha Zanzibar kitapata uwezeshaji wa kifedha moja kwa moja kutoka
CAF na FIFA kwa ajili ya timu ya taifa.
Tags
MICHEZO KIMATAIFA