KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki
na Kati, Azam FC, usiku huu imetinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho
(Azam Sports Federation Cup) kwa kishindo baada ya kuipiga Ndanda mabao
3-1, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Shujaa wa Azam FC katika mchezo
huo alikuwa ni mshambuliaji kinda Shaaban Idd, aliyefunga mabao mawili
huku jingine likisukimizwa wavuni na Ramadhan Singano ‘Messi’.
Azam FC iliuanza mchezo huo kwa
kasi ikicheza soka la kasi na kufanya mashambulizi matatu ya hatari na
kufanikiwa kupata bao la uongozi dakika ya 13, lililofungwa na Shaaban
aliyemzidi maarifa kipa wa Ndanda, Jeremiah Kisubi.
Dakika moja baadaye Ndanda
alisawazisha bao hilo kupitia kwa William Lucian, aliyepiga shuti la
moja kwa moja baada ya kipa wa Azam FC, Aishi Manula, kuokoa mchomo
mkali wa nguvu kwa ngumi uliokuwa umeelekezwa langoni mwake.
Dakika ya 17 Azam FC ilipata pigo
na kulazimika kufanya mabadiliko baada ya kuumia kwa beki wake, Yakubu
Mohammed, ambapo nafasi yake ilichukuliwa na David Mwantika dakika ya
20.
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na
Kombe la Mapinduzi msimu huu, walizidi kuendeleza kasi yao kwenye lango
la Ndanda, dakika ya 22 ilifanya shambulizi kali baada ya Salum Abubakar
‘Sure Boy’, kupiga pasi safi ya juu iliyookolewa vibaya na kipa, lakini
shuti alilopiga Frank Domayo, liliokolewa na mabeki.
Alikuwa ni Shaaban tena
aliyeendeleza kilio kwenye lango la Ndanda, baada ya kufunga Azam FC bao
safi dakika ya 44 kufuatia kuwazidi ujanja mabeki na kuunyanyua mpira
uliompita kipa na kujaa wavuni na kufanya Azam FC iende mapumziko ikiwa
kifua mbele kwa mabao hayo.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi
na ndani ya dakika ya kwanza ya kipindi hicho, Singano aliyekuwa kwenye
kiwango bora hivi sasa aliihakikishia ushindi Azam FC kwa kufunga bao
zuri baada ya kupiga krosi iliyojaa moja kwa moja wavuni.
Hilo ni bao la tatu la Singano
ndani ya mechi nne zilizopita za michuano yote, mengine akifunga kwenye
mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano hiyo Azam FC ilipoifunga Mtibwa
Sugar 1-0, huku pia akitupia walipopata ushindi kama huo dhidi ya
Mbabane Swallows.
Ushindi huo unaifanya Azam FC kuwa
kwenye nafasi ya kukutana na timu nyingine kama vile Mbao, Simba ambazo
nazo zimetinga hatua hiyo au mshindi wa mchezo mwingine wa robo fainali
kati ya Yanga na Tanzania Prisons utakaofanyika Aprili 22.
Mara baada ya mchezo huo kikosi
cha Azam FC kitakuwa na mapumziko kesho Alhamisi kabla ya kurejea tena
mazoezini keshokutwa Ijumaa kuanza maandalizi ya kujiandaa na mchezo
ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mtibwa Sugar
utakaofanyika Uwanja wa Manungu, Morogoro Jumatatu ijayo.
Chanzo: azamfc.co.tz
Tags
MICHEZO KITAIFA