Bunge limeelezwa kuwa, Wizara ya Nishati na Madini inahitaji Sh2 bilioni
kwa ajili ya kusambaza gesi majumbani katika mikoa ya Lindi, Mtwara na
Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema jana kuwa,
mradi wa usambazaji gesi unaweza kukamilika ifikapo mwezi Julai.
Dk Kalemani alitaja kiasi kamili cha gesi kinachohitajika kwenye nyumba
za watu katika mikoa hiyo ni mita za ujazo kati ya milioni tano hadi 10
ambazo uwezekano wa kupatikana ni mkubwa kwa kuwa gesi ipo ya kutosha.
Naibu waziri huyo alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtwara
Mjini (CUF), Maftaha Nachuma aliyetaka kujua kiasi na gharama
zitakazotumika kwa ajili ya usambazaji majumbani.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua ni lini Serikali
itasitisha usafirishaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda Kinyerezi Dar es
Salaam, ili wananchi wa Mtwara waweze kunufaika kwanza na ajira
zitokanazo na uchakataji wa gesi hiyo asilia na kujenga viwanda.
Hata hivyo, naibu waziri alisema sera mpya ya nishati ya mwaka 2015 na
Sera ya Gesi ya mwaka 2013 zinalenga kutoa fursa ya gesi asilia
kuwanufaisha Watanzania wote, ikiwa ni pamoja na wananchi wa eneo
inakopatikana rasilimali hiyo.
Alisema kuna miradi miwili inayosafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na
Lindi hadi Dar es Salaam. Dk Kalemani alisema mradi mmoja ni mpya
unaosafirisha gesi kutoka Mtwara ambao ulikamilika mwaka 2015, huku
mwingine ni wa Songas uliokamilika mwaka 2004 wakati gesi inayochakatwa
Madiba, Mtwara inasafirishwa kwa bomba kwenda Mkuranga.
Alisema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
inatekeleza mradi wa kuunganisha gesi hiyo katika Kiwanda cha Dangote
kilichopo Mtwara ambacho kitahitaji takriban futi za ujazo 45 milioni.
