Wakati wabunge saba kati ya tisa watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge
la Afrika Mashariki (Eala) wakipatikana juzi usiku, suala la
wawakilishi wa upinzani limetawaliwa na hali ya kutoeleweka, huku
ikibainika rasmi kuwepo kwa CUF “A” na CUF “B”.
Kikao cha juzi kilichotawaliwa na mjadala wa kikanuni kuhusu wawakilishi
wa Chadema na CUF, kiliweka rekodi ya kuchukua muda mrefu baada ya
kumalizika saa 7:00 usiku kikikipiku kikao kilichojadili sakata la
uchotwaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Bunge lilichagua wanachama sita wa CCM kuingia Bunge la Afrika
Mashariki, pamoja na mmoja kutoka CUF, ambaye amezua mjadala baada ya
jina lake kukubaliwa na msimamizi wa uchaguzi licha ya kusainiwa na
naibu katibu mkuu wa chama hicho badala ya katibu mkuu ambaye
aliwasilisha jina jingine.
Waliopitishwa ni Fancy Nkuhi, Happines Legiko, Maryam Ussi Yahya, Dk
Abdullah Makame, Dk Ngawaru Maghembe na Alhaj Adam Kimbisa kutoka CCM,
wakati Habib Mnyaa, aliyekuwa amevuliwa uanachama na CUF, alichaguliwa
pia kuingia kwenye chombo hicho.
Hata hivyo, wanachama wawili walioteuliwa na Chadema kuwania ubunge wa
Eala, Ezekiah Wenje, aliyepata kura 124 za ndiyo na 174 za hapana, na
Lawrence Masha, aliyepata kura 124 za ndiyo na 198 za hapana,
hawajaingia kwenye chombo hicho, kitu ambacho kimeifanya Chadema kuamua
kwenda mahakamani.
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema jana
kuwa uchaguzi huo ulikuwa ni batili kutokana na taratibu kutofuatwa.
Pia, hoja ya kuwepo kwa CUF A na B iliyozungumziwa na Katibu wa Bunge,
Dk Thomas Kashililah ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi huo imeibua
mvurugano kwa chama hicho ambacho kimekuwa na mgogoro na mwenyekiti
wake, Profesa Ibrahim Lipumba tangu alipojiuzulu mwaka juzi na
kujirejesha mwaka jana.
CUF na pande mbili
Katika uchaguzi huo uliofanyika bungeni mjini Dodoma, CUF ilipeleka
wagombea wanne baada ya upande wa Profesa Lipumba kutuma majina matatu
huku upande wa Maalim Seif ukipeleka jina moja.
Majina yaliyopelekwa na upande wa Profesa Lipumba ni Mnyaa, Thomas
Malima na Sonia Magogo huku upande wa Maalim Seif ukipeleka jina la
Twaha Taslima.
Kitendo cha Dk Kashililah kutangaza kukubali majina ya pande zote mbili,
kilifanya wabunge waanze kuhoji sababu za ofisi ya Bunge kukubali
kupokea majina ambayo hayajasainiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif
Sharif Hamad.
Akihoji suala hilo, Lissu alisoma barua ambayo ofisi ya Bunge
ilimwandikia Maalim Seif kuthibitisha kupokea jina la Taslima na
kuandika kasoro ambazo zilionekana katika fomu, akisema huo ni
uthibitisho kuwa Maalim Seif ndiye katibu wa chama hicho.
Alihoji sababu za kupokea fomu za upande mwingine wakati Maalim Seif
yupo. Spika John Ndugai alisema hana taarifa za mawasiliano hayo na
hivyo kumtaka katibu atoe maelezo.
“Nafikiri anachokisoma (Lissu) ni sahihi na tuliandika. Msingi wa
andiko letu ulitokana na barua ya tarehe 28 Machi kutoka Tume ya Taifa
ya Uchaguzi,” alisema Dk Kashililah wakati akitoa maelezo.
“Hatukuviandikia vyama kuviomba, tulitoa GN 376, vyama viliandika
vikaomba. Mimi sikuvitambua, aliyevitambua vyama ni mkurugenzi wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi. Ninayo orodha ya CUF “A” wamewasilisha kupitia kwa
naibu katibu mkuu, na CUF “B” kupitia kwa katibu mkuu.
“Mheshimiwa Spika ni vizuri tuelewane. Katika barua ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ndipo viongozi wawili wa CUF wanapokutana na wala si ofisi ya
msimamizi wa uchaguzi.
"Mimi nieleze wazi. Kwani aliyepeleka jina la Mnyaa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ni nani? Na aliyepeleka jina la Taslima ni nani? Sasa mbona
wote wameleta?”
Hivi karibuni Profesa Lipumba alitangaza kumteua Sakaya kukaimu nafasi
hiyo, akisema Maalim Seif hatii maagizo. Kwa mujibu wa katiba ya CUF,
katibu mkuu huchaguliwa na mkutano mkuu wa chama.
Akieleza utaratibu wa kuwathibitisha wagombea wa Eala, Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa Nec, Ramadhani Kailima alisema walipokea majina ya wagombea
kutoka vyama vya siasa na kwa suala la CUF hawajui kuhusu mgogoro
unaoendelea.
“Sisi hatupitishi majina ya wag- ombea. Soma taarifa ya Spika kwenye GN
(Gazeti la Serikali). Kazi yetu ni kuthibitisha wagombea. Mimi sijui
kama kuna mgogoro CUF. Tena andika kwa wino mweusi kabisa,” alisema
Kailima.
“Sifa ya mtu kugombea ubunge ni lazima atokane na chama cha siasa na ni
lazima awe raia wa Tanzania. Sasa kama amedhaminiwa na Maalim Seif au
Lipumba, sisi hatujui kama kuna mgogoro.
“Mwenye jukumu la kusajili chama ni Msajili wa Vyama vya Siasa na
akishasajili anawasiliana na taasisi nyingine. Kwa hiyo sisi tunaangalia
uongozi alioutambua. Nec inaangalia sifa ya mtu kuwa mbunge, vyama vya
siasa kama CCM, CUF Chadema ndiyo wanatuletea majina,” alisema Kailima.
Alipoulizwa kuhusu katibu aliyetakiwa kutia saini za wagombea wa CUF, Kailima alisema Nec haifungwi na mgogoro uliopo.
“Tume haifungwi, tunawasiliana na mwenyekiti au katibu. Mwenyekiti wa
chama anawasiliana na mwenyekiti wa Tume na katibu mkuu anawasiliana na
mkurugenzi wa uchaguzi,” alisema.
“Ninyi si mliandika kuwa Magdalena Sakaya ameteuliwa kuwa kaimu katibu
mkuu wa CUF na msajili akaridhia? Sisi tunawasiliana na huyo huyo pia.
“Lipumba anawasiliana na mwenyekiti wa Tume na Maalim Seif anawasiliana na mimi mkurugenzi.”
Akizungumzia kuhusu wagombea watatu wa CUF, Sakaya ambaye pia ni mbunge
wa Kaliua, alisema alitia saini fomu zao kama kaimu katibu mkuu.
“Majina yalipelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuthibitishwa kisha
yakapelekwa Idara ya Uhamiaji kuthibitisha uraia ndipo yakapelekwa kwa
katibu wa Bunge,” alisema Sakaya.
“Fomu zao nilitia saini mimi kama kaimu katibu mkuu kwa sababu katiba
yetu inasema kama katibu mkuu hayupo, nafasi yake inakaimiwa na naibu
katibu mkuu.”
