
RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeanika
madudu ya mkataba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwenye mradi
wa Mlimani City.
Madudu hayo yanaonyesha namna chuo hicho kinavyopoteza mamilioni ambako amependekeza mkataba huo ufanyiwe marekebisho.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni, ujenzi
wa mradi wa Mlimani City ulianza Oktoba Mosi mwaka 2004, ukikadiriwa
kukamilika Septemba Mosi mwaka 2016.
Hata hivyo, CAG ameshauri yafanyike marekebisho katika baadhi ya vifungu vya mkataba huo.
Ripoti hiyo inaonyesha kwamba moja ya sababu ya kukiukwa maeneo ya mkataba wa wabia hao wawili ni uzembe wa menejimenti ya chuo.
Ripoti inasema: “Tulibaini kwamba mradi mdogo wa hoteli ya nyota tatu
(ambayo ina vyumba 100 kikiwemo chumba cha mikutano kinachochukua watu
1,000) na uboreshaji wa bustani ya botania, ikiwa ni sehemu ya mradi wa
Mlimani City, haujakamilika kwa kipindi cha miaka 10 tangu tarehe ya
makubaliano ya kumaliza mradi.
“Mtazamo wangu ni kuwa hakuna ufuatiliaji wa karibu, usimamizi na
tathmini ya mkataba huo kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Kwa sababu hiyo kuna uwezekano wa kushidwa kumalizia kazi iliyobaki kwa
sababu ya ongezeko kubwa ya gharama ya kumalizia mradi tangu kipindi
kilichopangwa kupita.
“Menejimenti ya Chuo Kikuu inashauriwa kuuangalia upya mkataba
iliouingia na Mlimani City Holding, kuharakisha umaliziaji wa miradi,”
ilieleza ripoti hiyo ya CAG.
Ripoti hiyo pia inaainisha ukiukwaji wa ulipaji wa ada ambayo mwekezaji anatakiwa kuitoa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa kifungu cha 1.1(j) cha mkataba pamoja na kifungu 10.1 cha
hati ya ukodishaji wa uwanja, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinapaswa
kipate asilimia 10 ya mapato ya kodi ghafi.
“Kinyume na kufungu tajwa hapo juu, Mlimani Holding Limited (MHL),
hufanya hesabu za gawio la kodi ya Chuo Kikuu kwa kuzingatia asilimia 10
ya mapato ya kodi baada ya kutoa gharama za uendeshaji badala ya
kujumuisha gharama za uendeshaji.
“Ukiukwaji huu unakifanya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa katika
hatari ya kupoteza kiasi kikubwa cha mapato kutoka katika mradi wa
Mlimani City,” inasema ripoti hiyo.
CAG anaishauri menejimenti ya chuo hicho ifanye upya hesabu za gawio
lake la asilimia 10 kutokana na mkataba na kuomba kulipwa na mpangaji
kiasi kilichokuwa kimekosewa.
Pia alishauri kuwasiliana na mpangaji na kufikiria kubadilisha mkataba
kuweka vifungu ambavyo vitaruhusu idara ya ukaguzi ya ndani ya chuo
kuangalia mapato na gharama za uendeshaji za mradi.
Ripoti hiyo pia imeainisha udhaifu wa ufuatiliaji na usimamizi wa mapato kutoka kwa wapangaji wadogo kwenye mradi huo.
Inasema kifungu cha 11.2(l) cha hati ya makubaliano, mpangaji (MHL)
anapaswa kutopangisha mtu yeyote ambaye hajathibitishwa na Mpangishaji
(Chuu Kikuu cha Dar es Salaam), ikiwa ni njia ya kudhibiti mapato yake.
Kinyume na makubaliano ya hayo, ukaguzi wa CAG umebaini kwamba MHL
amepangisha majengo kwa wapangaji wengine bila kupata kibali cha Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
“Kuna upungufu wa utekelezaji wa vipengele vya mkataba kwa upande wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivyo kusababisha Chuo kushindwa kujua kwa
usahihi mapato ya kodi kutoka kwa wapangaji wote.
“Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam inashauriwa kutekeleza
vifungu na vipengele vyote vya hati ya makubalian ya upangaji kikiwamo
kifungu 11.2 (l) cha hati ya makubaliano ambacho kinakitaka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam kuwathibitisha wapangaji wadogo wadogo,” anashauri
CAG.
Ripoti hiyo pia inaonyesha mapitio ya mkataba wa upangishaji wa ardhi
kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mlimani Holding Limited
yamegundua kwamba mkataba haumpi mmiliki wa ardhi haki ya kukagua kazi
zinazofanywa na mpangaji.
“Katika hali hii, mpangishaji, ambaye ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
hawezi kujua endapo mpangaji, Mlimani Holding Limited, anakiuka mkataba
katika uendeshaji au kuna baadhi ya wapangaji wa nyumba hawawekwi wazi
na mpangaji huyu,” inasema ripoti.
CAG anashauri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwasiliana na Mlimani
Holding Limited kupata haki ya kukagua shughuli za miradi kwa manufaa ya
pande zote mbili.
Ripoti hiyo inasema pia kwamba mapitio ya mkataba yamegundua mkataba huo
hauelezei hali halisi ya ugawanaji mali mkataba utakapoisha (miaka 50
au 85 kutokana na makubaliano ya pande mbili).
“Hakuna makubaliano yoyote yanayoelezea mgawanyo wa mali na miondombinu itakayokuwapo wakati mkataba unaisha.
“Kwa hali hii, kuna uwezekano wa kutokea mvutano wa sheria mwisho wa
mkataba. Hali hii ikitokea, Chuo Kikuu kitakosa msaada wa sheria.
“Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, unashauriwa kuingia katika
mazungumzo na Mlimani Holding Limited kuweka vifungu vitakavyoonyesha
haki ya kila upande wakati wa mkataba utakapoisha,” anaeleza CAG.
Ripoti hiyo pia inasema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( kiliingia katika
makubaliano na kampuni ya Ernest and Young kufanya ukaguzi maalumu kujua
kiasi cha mapato ambacho kinaidai kampuni ya Mlimani Holding Limited
katika kipindi cha Mei Mosi mwaka 2006 mpaka Juni 30 mwaka 2014 na
kubaini kutolipwa dola za Marekani 57,607.
“Wakati wa ukaguzi niligundua kuwa kiasi cha Dola za Marekani 309,458
kilitakiwa kipokelewe na Chuo kutoka MHL, lakini usuluhisho wa hesabu
ulionyesha MHL ililipa Dola za Marekani 213,850 kupitia uhamisho wa
benki kwa njia ya eletroniki na kubakisha Dola za Marekani 57,607.
“Kuna ufuatiliaji duni kwa upande wa menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam katika kukusanya deni hilo. Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam inashauriwa kuongeza nguvu katika kufuatilia na kukusanya deni
wanalolidai MHL,” inasema ripoti hiyo.
Tags
CAG