Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na kukemea vikali kauli zinazotolewa
na viongozi au makada wa chama hicho wambao wametenguliwa na Rais Dkt
John Pombe Magufuli katika nafasi zao mbalimbali walizokuwa
wakishikilia.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa,
Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga aliyasema hayo juzi akizungumza Mjini
Iringa katika mkutano na wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyomo mkoani humo
ambao ni wananchama na pia viongozi wa chama hicho katika ngazi ya
matawi na kata.
Lubinga aliwataka makada hao walioteuliwa na kisha kutemwa na Rais Dkt
Mwagufuli ambaye pia ni Mwenyeketi wa CCM Taifa, kuacha kulalamika na
kupiga kelele badala yake wakubiliane na mabadiliko hayo kwa nia ya
kuheshimu maamuzi ya Ikulu kwa uamuzi uliochukuliwa dhidi yao.
Licha ya kuwa kiongozi huyo hakutaja majina ya viongozi aliowataka
kuheshimu maamuzi ya Ikulu, lakini ni dhahiri kuwa miongoni mwa
waliolengwa ni Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Moses Nnauye ambaye
alitenguliwa katika nafasi yake aliyokuwa ya Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo nafasi aliyoitumikia kwa kipindi cha miezi
15.
Nape alitenguliwa katika nafasi hiyo ikiwa ni saa chache tu tangu
alipopokea ripoti ya kuvamiwa kwa kituo cha Clouds Media Group ambapo
ripoti hiyo ilithibitisha kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ndiye
aliyehusika katika tukio hilo.
Nafasi ya Nape ilichukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria,
Dkt. Harrison George Mwakyembe ambaye naye nafasi yake ikajazwa na
Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Prof. Palamagamba Aidan John Kabudi ambaye
ni mbobezi katika taaluma ya sheria.
Mwingine ambaye licha ya kuwa hakuenguliwa na Rais moja kwa moja lakini
alionyesha kutoridhishwa na mchakato wa kuenguliwa kwake ndani ya CCM ni
aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shyrose Bhanji. Yeye
alienguliwa alipotaka kugombea kwa mara ya pili, na tangu hapo amekuwa
akilalamika kwa madai kuwa njia zilizotumika hazikuwa za haki.
Tags
CCM- ONYO
