Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimesema kuwa hakijapokea barua yeyote
kutoka bungeni ikiwataka kupeleka majina ya wagombea ubunge wa Afrika
Mashariki (EALA).
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Owen
Mwandumbya, amesema kuwa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kinasubiri barua ya maelekezo kutoka bungeni lakini mpaka sasa
hakijapokea.
Uchaguzi wa wabunge wa EALA uliingia dosari baada ya wagombea wa
Chadema, Lawrence Masha na Ezekiah Wenje kupigiwa kura za hapana hivyo
kukosa wawakilishi wa nafasi ya ubunge wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya
Nje wa Chadema, John Mrema amesema kuwa mpaka sasa hawajapata barua
kutoka kwa katibu wa bunge Dkt. Thomas Kashililah kuhusu hatua
wanazopaswa kuchukua.
“Tangu umalizike uchaguzi wa awali hatujapata taarifa zozote kutoka
Ofisi ya Bunge, tunasubiri barua kutoka kwa Katibu wa Bunge mchakato
gani ufanyike ili suala hilo lifikie muafaka,”amesema Mrema.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema kuwa kama Chadema
watapeleka wagombea waliokataliwa basi wategemee majibu yale yale na
kwamba atalazimika kutumia utaratibu mwingine.
