Miaka tisa baada ya kuvuliwa upadri wa Kanisa Katoliki, Privatus
Kargendo jana alifunga ndoa na mchumba wake Rose Birusya. Ndoa hiyo
ilifungwa katika Kanisa la Mtakatifu Petro jijini Dar es Salaam katika
misa iliyoongozwa na Padri Stefano Kaombe.
Kabla ya kuvuliwa upadri, Karugendo alikuwa Padri wa Jimbo la
Rulenge-Ngara kabla ya Papa Benedict XVI kumvua daraja hilo kwa madai ya
kukiuka maadili ya kanisa katoliki.
Septemba 14, mwaka 2008 Karugendo alitangazwa kuwa ni muumini mlei asiye
na daraja la upadri tena kupitia hati ya Papa yenye namba Protokali
4182/08.
Ingawa sababu za kuvuliwa kwake hazikuwekwa wazi kwa jamii zaidi ya
kusema amekiuka kanuni za kanisa hilo, watu wengi walihusisha tukio hilo
dhidi ya andiko lake kuhusu UKIMWI na matumizi ya mipira ya kiume
(condoms).
Baada ya kuvuliwa cheo hicho, Karugendo sasa ni mchambuzi wa masuala ya
kisiasa na kijamii katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo gazeti la
Mwananchi.
Waumini waliokuwamo katika misa ya ndoa hiyo, walimpongeza Karugendo na
kusema kuwa uamuzi wake wa kufunga ndoa katika Kanisa Katoliki
umeonyesha kuwa hana tatizo nalo licha ya kuvuliwa cheo hicho.
Mapadri wa Kanisa Katoliki hawaruhusi kuoa ikiaminika ili waweze
kujikita zaidi katika kushughulikia masuala ya kanisa bila kuwa na kitu
cha kuwaondoa humo ikiwa ni pamoja na familia.
Tags
Padri
