Wapinzani wawili katika mgogoro wa uongozi wa CUF, Maalim Seif Sharif
Hamad na Profesa Ibrahim Lipumba sasa wamefikia pabaya baada ya kuamua
kupambana kuichukua ofisi ya makao makuu iliyopo Buguruni.
Kwa sasa ofisi hiyo inatumiwa na Profesa Lipumba, ambaye uamuzi wake wa
kurejea madarakani mwaka mmoja baada ya kujiuzulu uenyekiti na nyadhifa
nyingine zote, unapingwa na kundi lililopanga kuzichukua ofisi hizo
Jumapili.
Jana, kundi linalompinga Profesa Lipumba lilitangaza kuwa litakwenda
ofisi hizo Jumapili kwa ajili ya kusafisha “kila kitu ambacho hakitakiwi
kiwepo”, lakini mwenyekiti huyo amesema ameshajiandaa kukabiliana nao
na ameripoti suala hilo polisi.
Profesa Lipumba alisema hayo jana, ikiwa ni siku moja tangu Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF) limtake ajitokeze kuzungumzia kitendo cha
walinzi wa CUF kuwashambulia waandishi wa habari waliokuwa kwenye
mkutano ulioandaliwa na viongozi wa chama hicho Kinondoni.
Profesa Lipumba alikuwa akiwajibu wabunge wa CUF wanaomuunga mkono
Maalim Seif waliowaambia wanahabari katika viwanja vya Bunge mjini
Dodoma jana kuwa wamepanga kwenda ofisi za Buguruni Jumapili ijayo na
wataungana na wanachama wengine kufanya usafi.
“Tulianza kufanya usafi soko la Buguruni, tukamalizia katika ofisi yetu.
Kwa hiyo katika hali nzuri, hatuhitaji wabunge wasumbuke kufanya usafi
siku hiyo,” alisema Profesa Lipumba
Profesa Lipumba alisema watu hao hawana nia ya dhati ya kufanya usafi,
bali wamepanga kufanya vurugu katika ofisi hizo kwa kushirikiana na watu
wa chama kingine cha upinzani.
“Wanataka kuleta vurugu ili CUF ionekane na taswira mbaya kwa
Watanzania. Naomba wanachama waepuke mtego huu, namshauri (Mbunge wa
Temeke, Abdallah) Mtolea akafanye usafi huo Temeke mbona kuna masoko
mengi tu machafu?” alisema.
Awali mjini Dodoma, wabunge wanaomuunga Maalim Seif walisema watakwenda na vifaa vya usafikuondoa kila uchafu watakaoukuta
“Wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao hawamkubali Profesa Ibrahim
Lipumba kuwa mwenyekiti, wameamua kwenda kufanya usafi kwenye ofisi zao
za Buguruni, ofisi kuu ya CUF Buguruni,” alisema Mtolea akiwa
ameambatana na wabunge wenzake katika mkutano na waandishi uliofanyika
chumba cha habari cha Bunge.
“Na hatua hii imekuja baada ya kuona ofisi ile inatumika vibaya. Imekuwa
ndio kijiwe cha wahuni kupanga matukio ya kihalifu. Kwenda kuvamia
mikutano, kwenda kuwavamia watu na kadhalika. Sasa sisi kama wanachama
tumeona hatuwezi kuiacha hali hiyo iendelee.”
Aliwataka wanachama kutoka maeneo ya Dar es Salaam, Pwani na mikoa mingine wafike kufanya usafi huo.
Alipoulizwa aina ya uchafu wanaoenda kuuondoa, Mtolea alijibu “ni kitu
chochote ambacho hakiko mahali pake” na kwamba hata Profesa Lipumba
hayuko mahali pake.
“Tangu Msajili amtambue Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti, hatujawahi
kwenda katika ofisi yetu ya Buguruni, matokeo yake ofisi hiyo imekuwa na
uchafu mwingi na kuwa pango la wahuni,” alisema Mtolea.
Alipoulizwa uwezekano wa kutokea vurugu, Mtolea alisema hawajiandai kufanya fujo, bali kufanya usafi.
Kuhusu kesi iliyopo mahakamani kuhusu mgogoro huo, alisema ile inapinga
msajili kumtambua Lipumba na haizuii kusafisha ofisi yao.
Alisema hawaendi kuteka ofisi hizo, bali wanakwenda kwenye ofisi zao hivyo hawahitaji kuomba ruhusa kwa mtu yeyote.
“Ofisi ni chafu, sisi tunataka tukaisafishe kwa sababu imekuwa sehemu ya
kupanga mipango mibaya kwa mustakabali wa chama,” alisema.
Akiweka msisitizo wa jibu hilo, Mbunge wa Chambani, Yusuf Salim Hussein alisema hakuna silaha ya moto inayoshinda nguvu ya umma.
Awali, wabunge hao walitoa tamko la kuunga mkono tamko la TEF kuhusu
kulaani kitendo cha wafuasi wa Profesa Lipumba kuwashambulia waandishi
wa habari.
Mnadhimu wa chama hicho na Mbunge wa Malindi, Ally Salehe alisema TEF
imetoa tamko zito la kutaka waandishi wa habari kufanya kazi kwa usalama
na uhuru.
“Na isiwe TEF tu, tunataka watu wote waliokerwa na tukio hilo watoe tamko la kulaani,” alisema.
Kuhusu tamko la TEF, Profesa Lipumba alisema atatoa tamko kuhusu suala hilo ifikapo leo.
“Mimi ni muumini wa demokrasia. Hapa ninavyoongea na wewe nipo katika
hatua ya mwisho ya kumalizia kuandika barua kuelekea TEF ambayo itafika
kati ya leo (jana) jioni au kesho,” alisema.
Hata hivyo, alisema mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano kwa umma, Abdul Kambaya alitoa tamko kuhusu tukio hilo.
Katika tamko lake, Kambaya alisema mmoja wa watu walioshiriki
kushambulia mkutano ni mlinzi wao na kwamba alikuwa katika doria
kudhibiti wanachama wanaofanya mikutano hotelini.
