Rais Dk. John Pombe Magufuli, ameiagiza Wizara ya Fedha kufuta mara
moja ajira za watumishi wa umma 9,932 waliobainika kughushi vyeti,
kwenye orodha ya malipo ya watumishi wa umma.
Akiongea leo mara baada ya kupokea ripoti ya uhakiki wa vyeti vya
watumishi wa umma mjini Dodoma, Rais Magufuli pia amewataka watumishi
hao kuondoka wenyewe na iwapo watakaidi wakamatwe na vyombo vya dola na
kushtakiwa.
Rais Dk. Magufuli pia ameziagiza mamlaka husika kujumuisha nafasi 9,932
za ajira ambazo zimeachwa wazi na watumishi wa umma walioghushi vyeti,
kwenye ajira mpya zaidi ya elfu 52 za serikali ili ziweze kuchukuliwa na
watu wenye sifa na uwezo wa kumudu nyadhifa zilizoachwa.
Akizungumza wakati akiwasilisha ripoti hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, amesema, kwa Mujibu wa
Kanuni na Sheria za nchi zinabainisha wazi kuwa mtu atakaebainika
kughushi vyeti au kutoa taarifa za uongo adhabu yake ni pamoja na
kifungo cha Jela.
Tags
RAIS MAGUFULI
