
Wakati mgogoro ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) ukizidi kutokota,
Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,
Profesa Ibrahimu Lipumba anadaiwa kutaka kumvuta aliyekuwa Katibu Mkuu
wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Wilbroad Slaa,
kujiunga na CUF.
Madai hayo yameibuka baada ya kuwepo kwa mawasiliano ya karibu kati ya
Prof. Lipumba na Dk. Slaa ambao kwa nyakati tofauti mwaka 2015,
walijiondoa kwenye vyama vyao kipindi cha mchakato wa kusaka mgombea
urais wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa).
Ingawa Dk. Slaa kaika mahojiano alikanusha habari za yeye kutaka
kujiunga na CUF, lakini habari zinasema kuwa mawasiliano kati ya Prof.
Lipumba amekuwa akihaha kumshawishi Dk. Slaa pindi atakaporejea nchini
ajiunge na CUF na kushika moja ya nafasi za juu za uongozi.
Taarifa za kuaminika zilieleza kuwa mawasiliano kati ya Prof. Lipumba
na DK. Slaa yanalenga kuboresha safu ya uongozi wa chama hicho kwa
kumpa wadhifa wa Ukatibu Mkuu au Umakamu Mwenyekiti licha ya kudaiwa
kwenda kinyume cha Katiba iliyoanzisha CUF.
Kwa mujibu wa katiba hiyo, nafasi za juu za uongozi wa chama hicho
zinatakiwa kuzingatia uwiano wa pande mbili za Muungano. Endapo
mwenyekiti anatoka Bara, Katibu Mkuu atatoka upande wa pili wa Muungano.
Baadhi ya wana CUF wanaomuunga mkono Prof Lipumba wamekiri kuwa kumekuwa
na mawasiliano ya wawili hao, huku wakisema hakuna anayejua kiini cha
kuimarika kwa mawasiliano hayo wakati huu ambapo CUF imepasuka katika
makundi mawili, moja likiongozwa na Katibu Mkuu Maalim Seif na jingine
lipo chini ya Lipumba.
Msemaji wa CUF inayoongozwa na Maalim Seif, Mbarala Maharagande, amesema
kuwa taarifa za kurudi kwa Dk. Slaa amezisikia japo hajui atajiunga na
chama gani.
“Labda wale watu wa Lipumba ukiwauliza wanaweza kukuhakikishia hilo. Kwa
nafasi ya katibu itakuwa ngumu kwa sababu katiba yetu hairuhusu, lakini
kuwa mwanachama anaweza. Nguvu ya Lipumba ilishapungua sana na wenye
chama chao (wananchi) watakwenda kukichukua na kumtoa ofisini kwa hiyo
kama anarudi Dk. Slaa kuja kuongezea nguvu upande huo inawezekana”.
alisema Maharagande.
Akizungumza kwa njia ya simu, Dk Slaa aliyekuwa Mbunge wa Karatu alisema
taarifa hizo si sahihi kwani alishaahidi kwamba hatarudi kwenye siasa
za vyama.
Alisema hawezi kuyumba kwenye uamuzi wake licha ya kukataa kuweka wazi
kwamba ni lini atarejeea nchini, alisisitiza kuwa msimamo wake wa
kuachana na siasa za vyama uko palepale.
“Maneno yangu hayayumbi, sitafanya siasa za vyama, nimeachana nazo.
Naomba msiniingize kwenye siasa uchwara, sizifanyi hizo… Saisa ni
ajenda. Hizo siasa za kishabiki zifanyeni nyinyi huko Tanzania, mimi
sifanyi ushabiki, hakuna mtu anayekula ushabiki, ndiyo maana siasa zangu
siku zote ni ajenda, Watu wanataka maji, wanataka chakula, wanataka
elimu bora, si ushabiki”
“Kwa miaka 20 niliyokuwa kwenye siasa sijawahi kufanya ushabiki,
nilitafuta ajenda na kuipanga mikakati kwa ajili ya wananchi” alisema Dk
Slaa alipozungumza na mwandishi wa habari hizi.
Alisema atasimama kupiga kelele kwa ajili ya Tanzania pale atakapoona
mambo yanakwenda kombo na atafanya hivyo kwa mustakabali wa Taifa si
siasa.
Septemba 25, 2015 akizungumza na wandishi wa habari kwa zaidi ya saa 2
kisha kutangaza kujitoa Chadema, alisema ni afadhali apotee kwenye
ulimwengu wa siasa duniani kuliko kumuunga mkono Lowassa.
Credit: TanzaniaDaima