Ikiwa ni takribani miaka mitano tangu Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto
Kabwe, avurugane na Chadema ambacho kilikuwa chama chake, sasa hali hiyo
inaonekana kurudi tena kupitia uchaguzi wa ubunge wa Afrika Mashariki
(EALA).
Tofauti na awali ambapo alikosana na Chadema na kufukuzwa uanachama
kutokana na kile kilichodaiwa ni kuandaa waraka wa mabadiliko ya 2013,
sasa hivi ubunge wa EALA unaonekana kumvuruga tena mwanasiasa huyo na
Chadema, baada ya kuandika barua kwa Spika wa Bunge akitaka utaratibu
uliotangazwa wa namna ya kupata wabunge ubadilishwe.
Utaratibu huo mpya uliotangazwa, unatoa nafasi kwa wabunge wa EALA kwa
mwaka 2017 kulingana na idadi ya wabunge wa kila chama kwenye Bunge la
Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa Mwongozo huo, kutokana na idadi ya wabunge wa vyama kwa
kila chama, CCM imepata nafasi za wabunge sita kwenda EALA, Chadema
mbili, CUF moja, huku ACT Wazalendo pamoja na NCCR Mageuzi, vikiwa
havina nafasi hata moja kwenye Bunge hilo la Afrika Mashariki, kutokana
na kuwa na mbunge mmoja kila kimoja, hivyo kutokidhi vigezo.
Kutokana na hali hiyo, Zitto ameliandikia Bunge barua kutaka Kamati ya
Kanuni za Bunge ikutane kujadili uchaguzi wa wajumbe wa Tanzania kwenye
Bunge la Afrika Mashariki.
Barua hiyo, ambayo baadhi ya wachambuzi wa siasa wanadai inalenga kutaka
utaratibu wa awali ubadilishwe ili chama cha Zitto (ACT Wazalendo),
kimwingize mwanachama wake, Profesa Kitila Mkumbo kugombea ubunge huo,
inasema mwongozo uliotolewa na Bunge umekwenda kinyume cha Mkataba wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wanasema endapo hoja ya Zitto ikikubaliwa, ni rahisi zaidi wagombea wa
Chadema wakakosa nafasi hizo na badala yake nafasi za upinzani
kuiwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki zikachukuliwa na
wagombea wa ACT na wale wa CUF.
Hali hiyo inaelezwa kuchangiwa na wabunge wengi kwenye Bunge la Jamhuri
wa Muungano wa Tanzania kuwa ni wa CCM, hivyo ni rahisi kuweka msimamo
wa kuwapigia kura wale wagombea wa ACT Wazalendo na wale wa CUF, badala
ya wale wa Chadema kutokana na hali ya kisiasa iliyopo nchini kwa sasa.
Barua ya Zitto ya Machi 28 iliyoandikwa kutokana na Tangazo la Bunge
kwenye gazeti namba 11 la Machi 17, lililotangaza uchaguzi huo na
masharti yake, ilisema mwongozo wa uchaguzi huo unavunja kanuni
mbalimbali na kwamba kitakachofanyika sasa kitakuwa ni uteuzi na siyo
uchaguzi.
Alisema pia mwongozo huo, mbali na kuvunja Mkataba wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, unataka suala la jinsi lizingatiwe kwenye wabunge wanaokwenda
kuiwakilisha nchi katika Bunge hilo.
Baada ya Zitto kuandika malalamiko hayo, Mwanasheria wa Chadema, John
Malya, naye aliyajibu akirejea hukumu mbili za kesi ya Anthon Komu
(kwenye Divisheni ya Mwanzo na Divisheni ya Rufani).
Malya aliandika kwamba, mwongozo wa Ofisi ya Spika wa Bunge wa kugawa
idadi ya viti kwa vyama ni sahihi, kwa sababu Divisheni zote mbili za
Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki ziliamua.
Katika sehemu ya barua yake, alisema: “Mwenye kupaswa kubeba mzigo wa
makundi ya Zanzibar, Bara na Wanawake (ukiachilia mbali kundi la vyama
vya upinzani) ni chama chenye wabunge wengi (CCM)”.
Hoja hiyo ya Malya inachambuliwa na Ado Shaibu, ambaye aliandika ujumbe
unaogusa hoja za kisheria ambazo alitumia Malya kukosoa malalamiko ya
Zitto.
Shaibu alisema ni kosa kutumia kesi ya Antony Komu ambayo iliamuliwa na
Divisheni ya Mwanzo ya Mahakama ya Afrika Mashariki, lakini baadaye
Divisheni ya Rufani ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki ikatengua
hukumu hiyo kwa hoja ya kwamba Divisheni ya Mwanzo ya Mahakama haikuwa
na mamlaka ya kuamua suala husika.
