wanaokumbuka, siku hiyo shule zilifungwa, wafanyakazi serikalini
waliowahi kazini asubuhi walirudi nyumbani baada ya kuambiwa siku hiyo
ilikuwa sikukuu.
Kwa kifupi, siku hiyo – Septemba 6, 1966 — ilikuwa ni siku ya furaha kwa Watanzania.
Ni miaka zaidi ya 50 iliyopita siku Watanzania na wapenda uhuru na amani
duniani walifurahi bila kificho baada ya kupata habari za kufa kwa
aliyekuwa waziri mkuu wa Afrika Kusini, Hendrik Frensch Verwoerd,
aliyechomwa visu na Mzungu mwenzake aliyeitwa Dimitri Tsafendas.
Kaburu Verwoerd (hutamkwa Fevuat) ndiye mwasisi mkuu wa mfumo wa ubaguzi
wa rangi wa watu wa Afrika Kusini, kufuatana na rangi zao,
akatenga maeneo watu waishi kufuatana na rangi zao!
Hivyo, Weupe, Weusi, Machotara na Waasia wakaishi sehemu zao na Wazungu
(Weupe), waliokuwa hawafikii hata milioni mbili wakawatawala watu wa
rangi zingine waliokuwa zaidi ya milioni 30 wakati huo!
Weupe wakaamua kila kitu chini ya ubaguzi huo wa rangi uliolaaniwa
duniani ukijulikana kwa neno la Kikaburu la ‘apartheid’ ambao
ulianzishwa na Kaburu huyo mwaka 1948 hadi ulipoangamia mwaka 1994 mbele
ya walimwengu.
Verwoerd ndiye aliyekipandisha chama kikuu cha Makaburu cha National
Party (South Africa), hadi akawa waziri mkuu tangu Septemba 2, 1958
alipoongeza ukatili hususan dhidi ya weusi kupitia polisi, mashushushu
na jeshi la ulinzi.
Waliopinga ubaguzi walikamatwa, wakazuiliwa majumbani mwao, wakatupwa
magerezani, wakalazimika kuikimbia nchi hiyo, wakateswa au kuuawa ambapo
Verwoerd akaifanya nchi hiyo kuwa Jamhuri ya Afrika Kusini mwaka 1961.
Alivipiga marufuku vyama vya kupinga ubaguzi vya African National
Congress (ANC) na Pan Africanist Congress (PAC) na kuanzisha Mashitaka
ya Rivonia yaliyowatupa gerezani Mandela na wenzake.
Mzungu mmoja aliyeuchukia ubaguzi, David Pratt, alijaribu kumuua
Verwoerd Aprili 9, 1960, eneo la Milner Park, jijini Johannesburg.
Pratt aliyekuwa mkulima na mfanyabiashara, alimfyatulia Verwoerd risasi
mbili kutoka kwenye bastola, moja ikalichana vibaya shavu la kulia na
kulifumua sikio lake la kulia pia kabla ya walinzi na maofisa
kumnyang’anya bastola.
Verwowerd alianguka akivuja damu, akakimbizwa Hospitali ya Johannesburg
ambapo baada ya siku mbili madaktari walisema hali yake ilikuwa ya
kuridhisha na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Pretoria. Madaktari
walisema alipona kifo kimaajabu na walipomwondolea risasi walijua
asingeweza tena kusikia na kutembea bila kuyumba.
Hata hivyo, Mei 29 baada ya miezi isiyozidi miwili, alirejea kazini
akiwa mzima. Pratt alikiri alikuwa amedhamiria kumuua mwasisi huyo wa
ubaguzi wa rangi. Hata hivyo, alionekana na matatizo ya akili,
hakushitakiwa, akapelekwa hospitali ya magonjwa ya akili ambako Oktoba
1, 1961, siku ya 53 ya kuzaliwa kwake, alijinyonga.
Hata hivyo, miaka sita baadaye akiwa bado waziri mkuu, Verwoerd aliuawa
jijini Cape Town wakati anaingia Bungeni mchana saa 8:15 ambapo Dimitri
Tsafendas alimchoma visu mara nne shingoni na kifuani kabla ya kukamatwa
na wabunge na kukimbizwa hospitali alipofia njiani.
Kama ilivyokuwa kwa Pratt, Tsafendas naye alikwepa adhabu ya kifo kutokana na kuwa na matatizo ya akili.
Zulia lililokuwa na madoa makubwa ya damu ya Verwoerd baada ya kuuawa,
liliendelea kuwemo bungeni humo tangu wakati huo hadi lilipoondolewa
mwaka 2004.
Mazishi ya Verwoerd yalihudhuriwa na watu wapatao 250,000 wengi wao
wakiwa Wazungu, akamwacha mjane aliyefariki mwaka 2000 akiwa na umri wa
miaka 98.
